Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa pamoja na dunia
sasa kuweka mkazo ikiwemo ya kifedha kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia
nishati jadidifu kama vile jua, maji na upepo,
nchi za Afrika zinapaswa kutumia vyanzo ilivyonavyo kama vile makaa ya
mawe ili kuweza kuwa na umeme wa kutosha.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Februari 11, 2025, New
Delhi, India wakati akishiriki katika mjadala wa Mawaziri wa Sekta ya Nishati
kutoka India, Qatar, Uingereza na Tanzania wenye mada iliyosema Mpango Mpya wa Dunia wa
Biashara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Wiki ya Nishati India.
Dkt.Biteko
ametolea mfano kuwa Tanzania ina madini ya makaa ya mawe ya kutosha pamoja na
urani ambayo yanafaa kuzalisha umeme hata hivyo kumekuwa na changamoto ya kupata
ufadhili wa kuyaendeleza kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa vile yanatajwa
kusababisha uchafuzi wa mazingira akieleza kuwa makaa ya mawe yanaweza kutumika
kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kuondoa sumu ya kaboni.
Amesema kuwa
takribani watu milioni 600 barani Afrika hawajafikiwa na huduma ya umeme hivyo
kwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo makaa ya mawe
itawezesha lengo la kufikishia umeme watu hao kwa haraka.
“Afrika
inachangia uchafuzi wa mazingira kwa
kiasi kidogo kwa sababu ni bara maskini
lakini inatajwa kuwa na mchango sawa na mataifa mengine, mabadiliko ya matumizi
ya nishati hayakwepeki, nchi ziruhusiwe kuwa na uendelezaji endelevu wa
rasilimali zake kwa ajili ya kuwa na usalama
wa nishati,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza “Lazima
tuangalie ukweli na hali halisi mfano Qatar au India hali yao ya upatikanaji
umeme ni tofauti na Tanzania, hatutaweza
kutumia njia ya aina moja kwa ajili ya kutatua changamoto za masuala ya umeme
kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni lazima kutumia njia tofauti.”
Ameangazia
lengo la Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi Afrika (Mission 300) uliofanyika
nchini Tanzania hivi karibuni wa kufikisha nishati ya umeme kwa watu milioni
300 barani humo ifikapo mwaka 2030 na kusisitiza kuwa pia Afrika inahitaji
fedha na miundombinu ya kusafirisha umeme pamoja na vyanzo mseto vya uzalishaji
umeme ili kufikisha lengo la kuwapatia umeme wananchi wake kwa asilimia 100.
Pamoja na
hayo, Dkt. Biteko amebainisha mafanikio ya sekta ya nishati nchini Tanzania na
kusema kuwa kuna umeme wa kutosha huku ziada ikiwa ni megawati 750 na kwamba
imejenga miundombinu ya kusafirisha na kuunganisha umeme na nchi jirani kama
vile Kenya, Burundi na Rwanda ili kuwezesha biashara ya umeme.
Waziri
anayeshughulikia masuala ya nishati kutoka Uingereza, Mhe. Ed Milliband
ameipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika uzalishaji na usambazaji
umeme kwa wananchi na hasa miradi ya umeme kwenda katika nchi jirani.
Kwa upande
wake, Waziri wa Petroli na Gesi kutoka nchini India, Mhe. Hardeep Singh Puri
amesema kuwa Mkutano huo wa Nishati India unalenga kuwakutanisha pamoja
viongozi wa sekta ya nishati, watunga sera na wavumbuzi kutoka maeneo
mbalimbali duniani ili kujadili changamoto zilizopo katika sekta hiyo na
kutafuta suluhushi kwa mustakabali endelevu wa upatikanaji wa nishati.
Aidha,
utaangazia teknolojia za kisasa, mipango kabambe ya kupunguza uzalishaji kaboni
na fursa za uwekezaji zinazoendana na malengo ya nishati kimataifa.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni