Uwepo wa
Kituo cha Mfano cha Katente katika Mkoa wa Kimadini Mbogwe umeleta mapinduzi
katika ukusanyaji wa Maduhuli ya
Serikali kufuatia Wachimbaji Wadogo wa Madini kukitumia
kituo hicho kuchenjua mawe yao jambo ambalo limewezesha ukusanyaji wa
kodi mbalimbali na kuongeza tija kwenye
uzalishaji wa madini ya dhahabu.
Hayo
yamebainishwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe Mhandisi
Jeremiah Hango wakati akizungumza na Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Madini Ofisini kwake Februari 10, 2025, waliotaka kufahamu manufaa ya
uwepo wa kituo hicho kwenye shughuli za uchimbaji mdogo.
Alisema
katika kipindi cha miaka mitatu, Mkoa huo wa kimadini umeshuhudia mafanikio
kutokana na kusogeza huduma kwa wachimbaji ikiwemo kituo hicho na hivyo
kupelekea mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji mdogo kuongezeka ambapo
katika Mwaka wa Fedha 2021/22 mkoa huo ulikusanya shilingi bilioni 21.3, Mwaka
wa Fedha 2022/23 shilingi bilioni 22.4
na Mwaka wa Fedha 2023/24 kiasi cha
bilioni 27.1 kilikusanywa.
‘’Tangu
kuanza mwaka huu wa fedha tayari tumekwishakusanya shilingi bilioni 18 na kwa mwenendo huu tunaamini tutavuka malengo
ya makusanyo tuliyoweza kukusanya katika kipindi kilichopita," amesema
Mhandisi Hango na kuongeza kwamba, mwaka huu wa fedha mkoa huo umepangiwa
kukusanya shilingi bilioni 45.
Aliongeza
kuwa, Mkoa wa Kimadini Mbogwe ulioanzishwa mwaka 2021, ukisimamia wilaya tatu
ikiwemo Bukombe, Mbogwe na Nyang'hwale kwa lengo la kusogeza huduma kwa
wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake
mafanikio makubwa yameshuhudiwa.
Pia, alisema,
uwepo wa Kituo cha Mfano Katente ni muhimu kwa Mkoa wa Kimadini Mbogwe ambapo
wachimbaji wanapata huduma bora na za uhakika pamoja na kupata ushauri wa namna
bora ya utunzaji wa mazingira.
"Naomba
nitumie fursa hii kuwataarifu wadau wote wa Sekta ya Madini kukitambua na
kukitumia Kituo chetu cha Mfano Katente kina wataalamu wa kutosha na wenye
maadili hivyo niwahamasishe wachimbaji wote wa Mbogwe kupeleka material yenu
katika kituo hicho kwa ajili ya uchenjuaji salama na wenye tija," alisema
Mhandisi Hango.
Akizungumzia
changamoto ya mahitaji makubwa ya uchenjuaji kituoni hapo, alisema kutokana na
mahitaji ya wachimbaji, Serikali ina mpango wa kuongeza ukubwa wa kituo hicho
ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji.
Pamoja na mambo
mengine, alitoa wito kwa wananchi na wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji
zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani humo ikiwemo ujenzi wa mitambo ya
uchenjuaji (CIP), uuzaji wa vifaa vya uchimbaji, uchimbaji wenyewe, biashara ya
madini pamoja na shughuli mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa shughuli hizo.
Katika
kuwaendeleza wachimbaji wadogo, alisema tayari Serikali imetenga maeneo kwa
ajili ya wachimbaji wadogo na tayari Serikali imetoa leseni za uchimbaji zaidi
ya 300 na kuna baadhi ya maeneo mchakato wa upatikanaji wa leseni unaendelea na
kueleza kwamba, Serikali inaendelea kuthamini wachimbaji wadogo mkoani humo.
Vituo vya
Mfano vilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora
na wa kisasa wa madini usio athiri mazingira naunaohamasisha matumizi ya
teknolojia rahisi katika shughuliza uchimbaji mdogo. Hadi sasa kuna jumla ya
vituovitatu vya mfano vilivyoko katika maeneo ya Lwamgasa-Geita,
Katente-Bukombe na Itumbi - Chunya.
0 Maoni