Hifadhi ya
urithi wa utamaduni wa dunia ya Magofu ya Kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara
inaendelea kupokea makundi makubwa ya watalii kutoka Mataifa mbalimbali duniani
ambapo jana Februari 15, 2025
imeshuhudia meli ya kifahari ya kitalii (Le Bougainville) ikishusha jumla ya
watalii 149 Hifadhini humo, ikiwa ni meli ya 6 kutia nanga katika bandari ya
mjini wa Kilwa katika kipindi cha kuanzia Januari - Februari, 2025.
Kwa miongo
kadhaa kumekuwa na dhana kwamba wageni wengi wa nje hupendelea zaidi utalii wa
kuona wanyamapori kuliko aina nyingine ya utalii, lakini hivi karibuni dhana
hiyo imeanza kubadilika kwa kasi ambapo Tanzania imeanza kupokea wageni makundi
Kwa makundi wakitembelea katika maeneo ya malikale hususani Hifadhi ya urithi
wa utamaduni wa dunia ya Magofu ya Kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara iliyo
chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA.
Watalii
waliotembelea hifadhi hiyo leo wametokea Mataifa ya Marekani, Uingereza, Ubelgiji, Austalia,
Ireland, Seychelles, Ujerumani na Ufaransa huku wengine wakitokea Mataifa ya
Ujerumani, Israeli, Ureno na Canada.
Ujio wa meli
hizi za watalii wa kigeni kutoka Mataifa mbalimbali ni uthibitisho tosha kuwa
Hifadhi hiyo inazidi kuwa kivutio cha Kimataifa na kuwa miongoni mwa maeneo
muhimu kwa Sekta ya utalii nchini.
Sambamba na
hilo, ujio wa meli hizi pia unaendelea kudhihirisha juhudi kubwa za kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu
zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour zinazidi kuzaa matunda lakini
pia ni ishara ya mafanikio ya mikakati
ya Serikali katika kukuza Sekta ya utalii.
Na. Beatus Maganja - TAWA
0 Maoni