Wizara ya Maliasili na utalii Kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025,
imepewa kibali cha kuajiri jumla ya askari 578 kupitia Taasisi zake za
uhifadhi. Askari hawa pamoja na majukumu mengine watatumika katika
kushughulikia changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kwenye maeneo ya
wananchi ikiwemo Tunduru Kaskazini.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mhe. Hassan Zidadu Kungu
aliyetaka kujua Serikali itapeleka lini
Askari wa kutosha wa Jeshi la Uhifadhi Tunduru Kaskazini ili kumaliza
athari zinazosababishwa na Wanyama Pori wakali na waharibifu.
Mhe. Kitandula alisema kuwa Serikali inampango wa kuongeza
askari wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Askari waliopo sasa 18 hadi kufikia Askari
wa Jeshi la Uhifadhi 25 na Askari Wahifadhi wa Vijiji (VGS) kutoka 60 hadi 80.
Aidha, Sambamba na askari hao, serikali imepanga kuongeza vitendea kazi kwa ajili ya Taasisi za Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kusini ikiwemo magari 09, pikipiki 10 na ndege nyuki 05, kwa ajili ya kuwawezesha kuongeza ufanisi wa kukabiliana na wanyamapori wakali wilayani Tunduru ili kumaliza tatizo hilo.
Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
0 Maoni