Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa
mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi
ambapo itapokea mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26
Machi, 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani, Jacobs
Mwambegele leo tarehe 26 Februari, 2025 muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza
kikao cha tume kilichofanyika mkoani Morogoro.
Kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 18(1) ya Kanuni za Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, napenda kutoa taarifa kwa umma kwamba,
kuanzia kesho siku ya Alhamis tarehe 27 Februari, 2025 Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi itaanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo
ya uchaguzi, amesema Jaji Mwambegele.
Akifafaunua kuhusu muda wa kupokea maombi, Jaji Mwambegele
amesema maombi yote ya kugawa au kubadilisha jina la jimbo yawasilishwe Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26
Machi, 2025.
Jaji Mwambegele amesema Tume inatekeleza jukumu hilo kwa
mujibu wa ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
Na. 2 ya Mwaka 2024, ambapo Tume imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa
Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu
hilo la kuchunguza mipaka na kugawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya
uchaguzi linaweza kufanywa na Tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka
kumi.
“Kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba, kwa mara ya mwisho
Tume ilichunguza mipaka na kugawa majimbo ya uchaguzi katika Jamhuri ya
Muungano mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yalianzishwa, amesema.
Jaji Mwambegele amewakumbusha wadau wote wenye maombi
wahakikishe kuwa mapendekezo yanajadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya,
kisha yawasilishwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya kujadiliwa katika
Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa awasilishe Tume mapendekezo
yaliyopitishwa na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa pamoja na viambatisho
vyote.
Amesema vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu,
ambapo kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 na majimbo ya
vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.
Ameongeza kuwa, idadi ya watu itakayotumika ni ile
iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Jaji Mwambegele amevitaja vigezo vingine kuwa ni hali ya
kiuchumi ya Jimbo, ukubwa wa eneo la Jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo
moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya
makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa bunge, idadi ya Wabunge wa Viti
Maalum Wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya
eneo linalokusudiwa kugawanywa.
Amesema halmashauri zinazokusudia kubadili jina la jimbo zinatapaswa kufuata utaratibu kama ule unaotumika katika kuwasilisha maombi ya kugawa majimbo.
0 Maoni