Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa waislamu nchini
kuendelea kumcha Mungu na kutenga muda wa kujifunza na kuisoma Qur’aan Tukufu
ambayo itawafunza mambo mema yaliyoelekezwa na Mwenyezi Mungu.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Februari 9, 2025 jijini Dar es salaam wakati akizindua Mashindano Makubwa zaidi ya Qur’aan Tukufu
Ulimwenguni 2025.
“ Nawaomba
msivunjike moyo akitokea mwenye tafsiri tofauti nyie msivunjike moyo wala
kukatishwa tamaa bali mfanye mashindano haya yawe kinara na kuutangaza uislamu
katika ulimwengu,” amesema Dkt. Biteko.
Pia
amewahimiza kumuomba Mungu ili Qur’aan iwanyanyue na isiwabwage katika shughuli
mbalimbali wanazofanya kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema “ Qur’aan
Ikunyanyue, Isikubwage”.
Amesema
Qur'aan inatoa funzo kwa watu na kuwa
waasisi wake waliyaanzisha kwa
ngazi ya madrasa lakini baadaye kutokana na umuhimu wake yakavutia wengi zaidi
na kuwa mashindano ngazi ya mtaa, kata, wilaya, mkoa hadi kuwa ya Afrika Mashariki, Bara la Afrika na kisha
kufikia ngazi ya kuwa mashindano ya Ulimwengu.
“ Mashindano
haya mbali na kuwa yanachochea usomaji wa Qur’aan Tukufu na hivyo kujenga
uelewa wa hofu ya Mwenyezi Mungu lakini pia yanaitangaza Tanzania katika
taswira chanya,” amebainisha Dkt. Biteko.
Ameendelea
kusema kuwa Nabii Musa aliwalingania watu wake kwa kutumia muongozo kutoka
katika Taurati, Nabii Daudi yeye akatumia Zaburi, Nabii Issa (Yesu) akatumia
Injili na Mtume Muhamad swalla llahu alayhi wasallam akatumia Qur’aan tukufu
kuwalingania watu wa umma wake.
"Kimsingi
vitabu hivi vya muongozo vinamfundisha binadamu tabia njema na kumsihi
kuzishikilia na kumuonesha tabia zisizofaa na kumuasa kukaa mbali nazo.”
Dkt. Biteko
amerejea aya katika Qur’aan tukufu sura ya 35, Surat Faatir, aya ya 28 “… kwa
hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni”.
Amefafanua “
Aya hii ina maanisha kuwa wale waliopata ujuzi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu
ambayo yanapatikana katika Qur’aan tukufu na kuyazingatia yale waliyojifunza
ndio wanaofika daraja la uchamungu.”
Vilevile,
Dkt. Biteko ameipongeza Taasisi ya Al- Hikma kwa jitihada zake za kukuza
Mashindano ya kuhifadhi Qur’aan Tukufu ulimwenguni.
Mkurugenzi
Mkuu wa Al- Hikma na Mwenyekiti wa Mashindano ya Qur’aan Tukufu Ulimwenguni,
Sheikh Nurdin Kishk amesema kuwa
mashindano hayo yameendelea kukua kila
mwaka kutokana na mapenzi ya kuhifadhi Qur’aan.
Aidha,
ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake na kwa kuridhia mashindano hayo
kufanyika katika Uwanja wa Taifa mnamo Machi 16, 2025 ambapo Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi.
“ Mashindano
haya yanayofanywa na Al- Hikma Foundation yameweka alama ambayo haitafutika na
mataifa mbalimbali yameanza kuyaiga. Pia, Mashindano Makubwa Zaidi ya Qur’aan
Tukufu Afrika sasa yatajulikana kama Mashindano Makubwa Zaidi ya Qur’aan Tukufu
kwa Mabara yote ya Ulimwengu ,” amesema Sheikh Kishk.
Akizungumza kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ali Ngerukwa amesema kuwa Mufti Mkuu yupo tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo ya Ali- Hikma katika kutekeleza shughuli zao.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni