Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Kampuni zinazohusika na
Usambazaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) -TZLPGA kwa lengo la kuwashukuru kwa
mchango wao katika utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali
ikiwemo utatuzi wa changamoto
zinazoikumba TZLPGA ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa urahisi nchi nzima.
Mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Jumuiya hiyo yamefanyika
leo Februari 20, 2025 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja Watendaji kutoka.Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji ( EWURA) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA).
“Ili Serikali ifanikiwe lazima kuwashirikisha watu wake,
tunawashukuru sana kwa mchango wenu katika kufanikisha Mkakati wa Nishati Safi
ya Kupikia ambao kutoka tuuzindue mwaka 2024, uelewa na matumizi ya mitungi ya
gesi umeendelea kuongezeka, mitungi hii ni gharama lakini ninyi mnajitoa na
kutuunga mkono," amesema Dkt. Biteko.
Hata hivyo Dkt.Biteko amezitaka kampuni hizo kuhakikisha
huduma ya upatikanaji wa mitungi ya gesi
inafika kwa wingi hadi ngazi ya vijiji ili kuweza kufikia lengo la
kuhakikisha kuwa asilimia 75 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia
ifikapo 2030 ikiwa pia ni utekelezaji wa Mpango wa Mahsusi wa Nishati ( Energy
Compact uliosainiwa mwezi Januari 2025.
Amesema kuwa lengo la kikao hicho pia lilikuwa ni kujadili
changamoto ambazo kampuni hizo wanakutana nazo ikiwemo za kikodi ambazo zina
nafasi ya kujadiliwa katika Muswada wa Masuala ya Fedha utakaosomwa katika
Bunge la Bajeti la mwaka 2025/2026.
"Tumekutana hapa
ili tunapoelekea kwenye Bajeti ya Serikali mtuambie kipi tukiboreshe
kupitia Muswada wa Masuala Fedha na ni vizuri pia mkatueleza jambo gani lifanyike ili kurahisisha upatikanaji
wa huduma kwa wananchi,” ameeleza Dkt. Biteko.
Kuhusu Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia amesema kuwa, “Tangu
tulipozindua Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia tumepata
ushirikiano mkubwa sana Afrika na duniani kote kupitia diplomasia ya Rais, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan na tumeendelea kupata fursa kubwa ya kuonesha na
kuuelezea mkakati wetu, pia tunaalikwa na nchi mbalimbali hata ambazo zimepiga
hatua kuliko sisi, hii inaonesha kwa
vitendo dhamira yetu ya kuhakikisha watu wanahama kutoka kwenye matumizi ya
kuni na mkaa na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia," amebainisha Dkt.
Biteko.
Amesema mwaka 2021 idadi ya watumiaji wa Nishati Safi ya
Kupikia nchini ilikuwa asilimia 9 pekee. Aidha, wakati Mkakati huo unazinduliwa
Mei 2024 hadi Februari 2025 watumiaji
wamefikia asilimia 33 hivyo ni hatua
nzuri katika kufikia lengo la Serikali la kufikisha asimilia 80 ya watumiaji wa
Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.
Ameeleza kuwa changamoto inayoikabili Serikali katika
kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ni uwepo wa nishati
mbadala ambazo si safi za kuni na mikaa ukilinganisha na nchi zingine ambazo hazina urahisi wa
upatikanaji wa kuni na mkaa, hivyo ametaja mbinu ya kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni kuendelea kutoa elimu
mara kwa mara ili kusaidia wananchi kubadili
tabia na mitazamo juu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Jumuiya hiyo, hususan
kuhusu ombi la unafuu wa kodi katika bidhaa za gesi, amesema suala hilo
limepokelewa na litafanyiwa kazi na Serikali.
Vilevile, ameishauri Jumuiya hiyo kutumia vyombo vya habari
kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kulipia.
Aidha, ametoa changamoto kwa Jumuiya hiyo kutumia fursa ya
Bandari kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa mitungi ya gesi katika
Ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ni faida ya kichumi kwa nchi na pia kuwezesha
matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felschemi
Mramba amesema kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kuwa hifadhi maalum za
mafuta ambapo suala la hifadhi maalum ya mitungi ya gesi linaangaliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kampuni
zinazohusika na Usambazaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) nchini ( TZLPGA),
Hamisi Ramadhani amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuitisha kikao na Jumuiya
hiyo ili kujadili masuala ya kiutendaji ambayo yanalenga kuhakikisha kampuni
hizo zinaendelea kufanya biashara kikamilifu na gesi ya mitungi inapatikana
katka maeneo yote nchini kwa wakati wote.
Ramadhani amesema kuwa, kampuni zinazohusika na usambazaji
wa mitungi ya gesi zinapata ushirikiano mzuri kutoka Serikalini kupitia Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kutengeneza sheria
zinazoongoza biashara ya LPG, Wakala wa Nishati Vijjini ( REA) kwa
kutekeleza programu mbalimbali za Nishati Safi ya Kupikia na Shirika la Viwango
Tanzania ( TBS) kwa kuweka viwango (standards) zinazoongoza biashara ya LPG.
Ameipongeza EWURA pia kwa kuwa mdhibiti bora kwani mara zote
imekuwa ikisikiliza maoni ya wadau na kuyafanyia kazi kwa maslahi ya pande zote
mbili ambazo ni Serikali na Wafanyabiashara.
Ameongeza kuwa mitungi ya gesi imesambaa sana sehemu za
mijini kuliko vijijini hata hivyo kampuni hizo zinajitahidi ili biashara hiyo
iendelee kushamiri maeneo ya vijijini pia ikiwa ni jitihada za kuhakikisha
asilimia 75 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030.
Katika hatua nyingine, Jumuiya hiyo imesema ipo tayari
kushirikiana na Serikali ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa
LPG katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni