WAZIRI MKUU, Mhe.
Kassim Majaliwa amewasisitiza Watanzania wote kushirikiana na Serikali kuweka
mkazo kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kubadili utaratibu za
kupika chakula ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
“Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa kinara katika kuhamasisha
matumizi ya nishati safi ya kupikia. Suala hilo limempa heshima kubwa kimataifa
ikiwemo Mkutano wa 79 wa Baraza la Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi Septemba,
2024. Kama mtakumbuka kupitia mkutano huo, Mheshimiwa Rais alipongezwa kwa
jitihada zake za kuhakikisha malengo ya kuhamia kwenda nishati safi ya kupikia
yanatimia ifikapo mwaka 2030.”
Mhe. Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM
Taifa ametoa pongezi hizo leo (Jumapili, Januari 26, 2025) alipozungumza na
wananchi katika Mkutano Mkuu wa CCM jimbo la Katavi, mkoani Katavi uliofanyika
uwanja wa TARURA uliopo Inyonga wilayani Mlele.
“Huu ndiyo msukumo uliofanya Tanzania kuwa mwenyeji wa
Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Nishati Afrika utakaofanyika jijini Dar es Salaam
tarehe 27 hadi 28 Januari 2025. Lengo la mkutano huo ni kuhamasisha ushirikiano
mpana wa kufikisha nishati ya umeme kwa watu milioni 300 Barani Afrika ifikapo
mwaka 2030. Katika hili sote tunapaswa kumpongeza na kumuunga mkono Rais wetu.”
Wakati huo huo,
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya
elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, hivyo amewasisitiza wazazi, walezi na mamlaka
zote ikiwemo watendaji wa Mitaa na Kata wahakikishe uandikishaji wa wanafunzi
wa elimu ya awali na kidato cha kwanza unafanyika kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa amewataka Wana-CCM
kujiandaa na uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika
Oktoba 2025 kwa kuimarisha mshikamano na kueleza utekelezaji wa ilani. ”
Tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu ueleze tuliyoyafanya iwe kwa ngazi ya Kata,
jimbo viongozi tusimame imara. Tueleze utekelezaji wa Ilani.”
Amesema huu ni wakati muafaka wa kujiandaa na uchaguzi huo
muhimu ili kuhakikisha ushindi mkubwa unapatikana Wana CCM wote wana wajibu wa
kueleza yote yaliyotekelezwa kwenye maeneo yao kabla ya mgombea urais
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea Mwenza Mhe. Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi hawajafika katika maeneo yao.
Waziri Mkuu amesema Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo katika maeneo yao hivyo wakati utakapofika viongozi hao wa CCM wahakikishe wanakwenda kwa wananchi na kueleza namna miradi mbalimbali ilivyotekelezwa ikiwemo ya maji, elimu, maji, kilimo, miundombinu.



0 Maoni