Rais wa Benki ya Dunia (WBG), Bw. Ajay Banga amewasili
nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu
Nishati ujulikanao kama “Mission 300”, utakaofanyika tarehe 27 hadi 28 Januari
2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es
Salaam.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam Bw.Banga amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi kwa niaba ya Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt.
Natu Mwamba, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe.Dkt.Elsie Kanza, Mwakilishi
Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bw. Nathan Belete na Viongozi wengine waandamizi
wa Serikali.
Mkutano huo unalenga kuwakutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika na
wadau muhimu wa sekta ya nishati na fedha ili kujadili namna ya upatikanaji wa
nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa watu milioni 300 barani Afrika
ifikapo mwaka 2030.
Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu katika kusaidia
miradi ya upatikanaji wa nishati nchini na barani Afrika kwa namna mbalimbali
ikiwemo kufadhili miradi ya upanuzi wa gridi ya taifa, maendeleo ya nishati
mbadala, gridi ndogo na usaidizi wa sera, na kuwezesha ushiriki wa sekta
binafsi katika sekta ya nishati, huku ikilenga zaidi kuzifikia jamii ambazo
hazijafikiwa na huduma ya nishati.
Mbali na Rais wa Benki ya Dunia, Viongozi wengine Wakuu wa
Nchi na Mashirikia waliowasili nchini
hadi sasa ni Rais wa Jamhuri ya Sierra Leone, Mheshimiwa Julius Maada
Bio na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina.
Poja na mambo mengine mkutano huo unatarajiwa kuridhia na
kusaini Mpango Mahsusi wa Nishati Afrika (Africa Energy Compact), kusaini Awamu
ya kwanza ya Mipango ya Kitaifa ya Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025 –
2030 (National Energy Compacts) na kupitisha Tamko la Dar es Salaam la Mkutano
wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Dar es Salaam Declaration on Africa
Heads of State Energy Summit) ambao utajumuisha nchi 14 za Tanzania, DRC, Ivory
Coast, Burkina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Mozambique,
Niger, Nigeria, Senegal na Zambia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri katika sekta ya nishati, ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2024, uzalishaji umeme kwa Tanzania bara ulikuwa umefikia Megawati 3,169.20 ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 78.4 mwaka 2020. Wakati huohuo kupitia Mpango wa Usambazaji Umeme vijijini (REA), takriban vijiji vyote nchini vimefikiwa na huduma ya nishati ya umeme.




0 Maoni