Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa
kushirikiana na Kampuni ya Busybee imezindua Kampeni yake ijulikanayo Valentine
Weekend Gateway na TANAPA jijini Mwanza, lengo likiwa ni kuhamasisha Watanzania
na wasio Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa kipindi hiki cha msimu wa
Sikukuu ya Wapendanao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa
uzinduzi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo, anayeshughulikia Kitengo
cha Maendeleo ya Biashara TANAPA Makao Makuu, alianza kwa kufunga rasmi kampeni
ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA iliyozinduliwa Desemba 01, 2024 Jijini Arusha.
Kamishna Lyimo alieleza mafanikio ya kampeni hiyo kwa
kutaja ongezeko kubwa la watalii wa ndani: “Kampeni ya Shangwe la Sikukuu na
TANAPA ilifanikiwa kuvuka lengo la awali ambalo lilikuwa ni kupata watalii wa
Kitanzania na 28,000.”
Kamishna Lyimo Aliongeza: “Jumla ya Watanzania 36,933
walitembelea Hifadhi za Taifa kuanzia tarehe (1/12/2024 hadi 5/1/2025), sawa na
ongezeko la asilimia 44% ukilinganisha na Watalii waliotembelea katika kipindi
kama hicho kwa mwaka jana (1/12/2023 hadi 5/1/2024).”
Akizungumzia dhima ya uzinduzi wa kampeni mpya ya Valentine
Weekend Gateaway na TANAPA, Kamishna Lyimo alisema, “Leo tunazindua kampeni hii
kwa Hifadhi zote 21, tunawahamasisha Watanzania wote watembelee Hifadhi zetu
maana tumeandaa vifurushi rafiki vya bei nafuu vinavyomwezesha kila Mtanzania
kumudu gharama za kutalii msimu wa wapendanao.”
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk. Tutindaga
Mwakijambile, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, alitoa maelezo
kuhusu Kisiwa cha Saanane ambapo ni mahali pa kipekee kwa wapendanao. Mandhari
tulivu, fursa za kipekee za kupumzika, na shughuli mbalimbali za kuburudisha
zinazotengeneza uzoefu wa kukumbukwa milele.
Kamishna Dk. Tutindaga aliongeza, “tumejiandaa
kuwahudumia wapendanao, Watalii wataweza kutembelea Kisiwa cha Saanane chenye
msitu wa kijani uliosheheni miamba minene ya mawe iliyobanana, wanyama kama
Swala, Nyumbu, Simba, Mamba, na Ndege wa aina mbalimbali pamoja na mandhari
nzuri ya jiji la Mwanza.”
Mkurugenzi wa Kampuni ya Busybee, Baraka Nyororo,
alieleza kwa upana kuhusu ushirikiano na TANAPA katika kuandaa tukio hilo
adhimu katika jiji la Mwanza, ambapo Watanzania wengi wanatarajiwa kushiriki
kutembelea kisiwa hicho siku ya Februari 15, 2025
Baraka alisema, “Tutaandaa tukio la Usiku mzuri kwa
wapendanao ambapo watafurahia Night Excursion, Valentine Romantic Dinner,
Bonfire, Games, burudani ya Muziki, matembezi ya miguu pamoja na kutazama nyota
wakati wa usiku.”
TANAPA imeendelea kunadi na kutangaza vivutio vya utalii
vilivyopo katika Hifadhi za Taifa nchini hasa kupitia matukio ambayo
yamepelekea kupatikana kwa mafanikio yanayochangia kufanikisha adhima ya
Serikali ya kufikisha watalii milioni tano (5) na mapato ya dola bilioni sita
(6) ifikapo mwaka 2025.



0 Maoni