Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imekusudia kuendelea kuboresha
huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo huduma za uhamiaji nchini ili
kuharakisha maendeleo ya watu.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Januari 11, 2025 baada ya kuweka Jiwe la Msingi katika jengo la
Uhamiaji lililopo katika Wilaya ya Micheweni, Pemba ikiwa ni sehemu ya
shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofikia
kilele chake Januari 12, 2025.
Amesema Wazanzibari na Watanzania wana kila sababu ya
kujivunia maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar ambapo miradi mbalimbali imetekelezwa ikilinganishwa na
kipindi kilichopita.
“Mtakubaliana na mimi kwamba Serikali zote mbili
zinaendelea kufanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii. Maendeleo haya ni matunda ya viongozi na waasisi Hayati Abeid Amani
Karume na Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere,” amesema Dkt.
Biteko.
Amesema ujenzi wa Afisi na Makaazi ya watumishi wa Idara
ya Uhamihaji ni ushahidi kwamba Serikali imenuia kuboresha mazingira ya kazi
kwa watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama
Khatib amemshukuru Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa ya
maendeleo sambamba na kuimarisha demokrasia.
Amesema wakati Wazanzibari wakiendelea kujivunia faraja
zinazotokana na Mapinduzi, ni muhimu wananchi kujua na kufahamiana ili kulinda
usalama wa nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe.
Hamza Hassan Juma amesema maboresho yanayoendelea Wilaya ya Micheweni
yamewaondoa katika hali ya umasikini.
Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara na maji
utachochea upatikanaji wa ajira kwa wakazi na hivyo kukuza uchumi na maendeleo.
Ameitaka Idara ya Uhamiaji kwa siku zijazo, kutafuta
viwanja vya makazi tofauti na viwanja vya Afisi ili kulinda faragha za
watumishi wanapokuwa kwenye mazingira ya makazi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna
Makakala, amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha masilahi na mazingira ya kazi
kwa Maafisa Uhamiaji katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent
Bashungwa amesema Serikali itahakikisha mazingira ya kazi na utumishi ndani ya
uhamiaji ili waendelee kuboresha huduma kwa wateja.
0 Maoni