Shamba la Miti Sao Hill lililo chini ya Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania limetajwa kuwa chachu ya uhifadhi wa rasilimali misitu na
nyuki hususani katika wilaya ya Mufindi kutoka na shughuli mbalimbali
zinazofanyika na shamba katika sekta ya misitu na nyuki.
Akizungumza kuelekea ziara ya mafunzo inayotarajia
kufanywa hapo kesho na viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani
Geita, Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura amesema kuwa lengo ziara
hiyo ni kuona namna gani Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imefanikiwa katika
shughuli za uhifadhi zinazochagizwa na uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill.
"Shughuli za uzalishaji wa mazao ya misitu
umechangia kuwepo kwa maendeleo katika Wilaya ya Mufindi kwani mapato mengi
yanakusanywa kupitia kodi zinazolipwa hivyo tumekuja kuona na kujifunza kwa
namna gani sisi pia tutanufaika na uwepo wa shamba la Miti Silayo."
Akizungumza wakati wa mapokezi ya vuongozi hao, Kamishna
wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo
amesema Shamba la Miti Sao Hill limekuwa mfano mzuri wa uhifadhi hususani
katika uanzishaji wa mashamba ya miti katika maeneo mbalimbali nchini kwani
manufaa na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kimazingira yamekuwa
chachu katika maendeleo ya maeneo mengine.
Aidha ameongeza kuwa uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill
umekuwa na mchango mkubwa katika uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha mazao ya
misitu kutokana na uwepo wa malighafi zinazotumika kuzalisha mazao hayo na
kuchangia ukuaji wa mapato ya halmashauri za Wilaya, Mkoa na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mufindi Ndg.
Reuben Chongolo amesema kuwa viongozi hqo kutoka Wilaya ya Chato kupitia ziara
hiyo watatembelea katika eneo la shamba la Miti Sao Hill kuona shughuli za
upandaji wa miti na uchakati wa mazao ya misitu katika viwanda vinavyozalisha
mazao ya misitu vilivyopo wilayani Mufindi.
Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika kwa muda wa Siku mbili
ikihushisha viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Viongozi kutoka
Wilaya ya Mufindi, Wahifadhi kutoka Shamba la Miti Sao Hill pamoja na baadhi ya
viongozi kutoka umoja wa wavunaji wa Shamba la Miti Saohill kuanzia kesho
tarehe 12 Januari 2025.
0 Maoni