Askofu Dkt. Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ameimwagia sifa Ofisi ya Msajili wa
Hazina kwa mageuzi makubwa na ya haraka yanayoendelea katika usimamizi na
uendeshaji wa mashirika ya umma chini ya uongozi wa Bw. Nehemiah Mchechu,
Msajili wa Hazina.
Askofu Malasusa ametoa pongezi hizo leo, Januari 11,
2025, katika Ibada maalumu iliyoandaliwa na familia ya Bw. Mchechu mahususi
kwaajili ya kumshukuru Mungu kwa ulinzi na baraka za mwaka 2024 na kuomba
rehema na neema zaidi katika mwaka mpya wa 2025.
Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la KKKT, Usharika
wa Mbezi Beach, Dar es Salaam imefanikisha kukusanya zaidi ya Sh70 milioni ikiwa ni sadaka
maalumu ya ujenzi wa Kanisa.
Katika ibada hiyo iliyoendeshwa na Mchungaji Allen Mbiso
na kushirikisha familia, ndugu, jamaa na marafiki, ikiwemo baadhi ya watumishi
wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Askofu Malasusa alisema siku zote Bw. Mchechu
amekuwa mtu wa kuleta mabadiliko popote anapofanya kazi.
“Hata sisi hapa
kwetu kwa kipindi chote alichotumika kama Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na
Mipango, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, kisha Katibu wa Usharika wa Mbezi
Beach, daima amekuwa mtu wa mabadiliko,” alisisitiza Askofu Malasusa.
Kwa upande wake Bw. Mchechu akielezea sababu ya kuomba
misa hiyo maalumu ya shukrani alisema imekuwa ni utaratibu wa familia yake
kurudi katika madhabahu kushukuru kwa yote ambayo Mungu amekuwa akitenda katika
maisha yao.
Bw. Mchechu alitolea mfano wa hadithi katika biblia
takatifu, kitabu cha Luka 17:11
inayowahusu watu 10 wenye uhitaji waliobarikiwa na Yesu Kristo lakini ni mmoja
tu kati yao ndiye alierudi kushukuru kwa kile alichotendewa na kusema kila mtu
ana sababu ya kusema asante katika kila jambo.
Hadithi hiyo inaeleza kuwa Yesu akiwa safarini kwenda
Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya.
Alipokuwa anaingia
katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali
wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma”.
Alipowaona akawaambia, nendeni mkajioneshe kwa makuhani.
Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.
Mmoja wao alipoona
kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. Akajitupa chini
mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru.
Huyo alikuwa Msamaria. Hapo Yesu akasema, “Je, si watu
kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi? Hakupatikana mwingine aliyerudi
kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?”
Kutokana na
kitendo alichofanya mgeni huyo, Yesu alimwambia, “simama, uende zako; imani
yako imekuponya.”
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma
Ofisi ya Msajili wa Hazina.
0 Maoni