Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mh. Amina J.
Mohamed ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt.
Samia S. Hassan kwa mkakati wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia na
utafutaji madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu Amina Mohamed ameyasema hayo leo wakati wa
mkutano wa pembeni wa Mkutano wa Nishati alipokutana na Waziri wa Madini Mh.
Anthony Mavunde.
“Naipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Rais Samia
ambao umekuja na ubunifu mkubwa katika maeneo mbalimbali.”
Mpango wa kufanya utafiti wa kina kupitia Vision2030 ni
mpango ambao tunauunga mkono kwa kuwa una lengo la kubaini madini ambayo mnayo
na hivyo kujiapanga vyema juu ya uvunaji wa madini hayo.
Dunia hivi sasa ina mahitaji makubwa ya madini mkakati,Tanzania
imebarikiwa kuwa na madini hayo kwa uwingi hivyo suala la uongezaji
thamani,utunzaji wa mazingira na kulinda jamii zinazoishi katika maeneo ya
uchimbaji wa madini ni vyema yakazingatiwa wakati wa uandaaji wa mkakati maalum
wa uvunaji wa madini ya kimkakati.
“Umoja wa Mataifa kupitia programu zake mbalimbali za
utunzaji wa mazingira ipo tayari kuunga mkono jitihada hii kubwa ya serikali ya
Tanzania,” alisema Mh. Amina Mohamed.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Madini Mh. Anthony
Mavunde amesema kipaumbele cha sekta ya Madini kwa hivi sasa ni kufanya utafati
wa kina ili kuiwezesha nchi kupata taarifa za kiwango na ubora wa madini
iliyonayo.
Aliongeza kwamba, utafiti wa kina utaleta matokeo chanya kwenye maeneo ya kijamii na kiuchumi na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo ya Tanzania, kwakuwa pamoja na mafanikio yote ya kwenye sekta ya madini eneo ambalo limefanyiwa utafiti ni asilimia 16% ya eneo la nchi nzima.
0 Maoni