Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
wenye lengo la kuharakisha upatikanaji umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo
2030 (Mission 300) utakaofanyika tarehe 27 na 28 Januari jijini Dar es Salaam
yamefikia asilimia 95.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 15 Januari 2025 mara
baada ya kukagua maandalizi ya Mkutano huo katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Amesema Wakuu wa Nchi 54 kutoka Bara la Afrika
wanatarajiwa kushiriki pamoja na viongozi wengine ambao ni Mawaziri wa Fedha na
Nishati kutoka barani Afrika, Marais wa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya
Maendeleo Afrika (AfDB), pamoja viongozi kutoka Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya
Umoja wa Afrika ambapo kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na kukamilisha
ukarabati wa ukumbi wa JNICC.
“Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na usajili na
uthibitisho wa wageni ambao watakuja kwa ajili ya ushiriki na ukarabati wa
maeneo mengine yatakayotumika kwenye mkutano huu, nichukue nafasi hii
kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua iliyofikiwa na kuliweka
jiji kwenye mandhari ya kuvutia,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, Mkutano wa M300 umekuwa kivutio ambacho
kimewashawishi Wakuu wa Taasisi nyingi
za Kimataifa kuonesha nia ya kushiriki mkutano huo mkubwa katika Sekta ya Nishati.
Ameeleza kuwa, Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo
kumetokana na Diplomasia nzuri ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo
imezidi kuimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa na kupelekea WB na AfDB
kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano.
Ametaja sababu
nyingine ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu ni
mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya Nishati huku akitoa mfano wa mafanikio
katika usambazaji wa nishati vijijini.
Amesema vijiji vyote nchini 12,318 vimesambaziwa umeme na
Vitongoji 34,000 kati ya 64,274 vilivyopo nchini, tayari vimesambaziwa umeme.
Ametaja baadhi ya faida za mkutano huo kuwa ni pamoja na
kuongezeka idadi ya Watanzania
watakaounganishwa na umeme ifikapo mwaka 2030 hadi kufikia milioni 13.5 kutoka
milioni 5.2 ya sasa.
Ameongeza kuwa, katika mkutano huo nchi zitasaini
mikakati ya kuharakisha kusambaza umeme kwa wananchi ambayo itaeleza kwa kina
hatua gani zitachukuliwa chini ya mwavuli wa WB na AfDB.
Ameongeza kuwa, faida nyingine zitakazotokana na mkutano
wa M300 ni kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara na kuongeza
heshima ya nchi katika Duru za kimataifa na Tanzania kuwa Taifa linalopigiwa
mfano kwenye nyanja mbalimbali.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuupokea kwa
mikono miwili mkutano huo ambao kwa kiasi kikubwa unazidi kumheshimisha Rais,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea na hali ya
amani na utulivu kuelekea katika mkutano huo wa kihistoria kutoka nchi ipige
hatua kwenye Sekta ya Nishati kwani ni Mkutano Mkubwa wa kwanza kufanyika.
Vilevile ametoa
wito kwa Waandishi wa Habari kuutangaza Mkutano huo kwa Watanzania ili
waufahamu kwa kina na kufahamu fursa zilizopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert
Chalamila amesema maandalizi ya kupokea ugeni huo yako katika hatua za mwisho.
Amesema ili kufanikisha mkutano huo, baadhi ya mitaa itafungwa ili kuwezesha maonesho na utalii wa ndani ikiwa ni pamoja na utalii wa tiba.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni