Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza Watanzania
kuendeleza upendo mshikamano na kuvumiliana zikiwa nyenzo muhimu za kufikia
maendeleo na ustawi wa Taifa.
Dkt. Biteko amesema hayo Kijijini kwao Bulangwa, Wilayani
Bukombe Mkoani Geita alipojumuika na maelfu ya wananchi katika hafla ya
kuukaribisha mwaka mpya 2025.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan imefanya mambo mengi makubwa na mazuri ambayo yanahitaji kuenziwa
na kuendelezwa ili kupata maendeleo ya kweli.
"Maono ya Rais Samia yamewezesha upatikanaji wa
maendeleo katika sekta mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu ya barabara,
shule, vituo vya Afya na maji na hatua hii imetambuliwa kitaifa na kimataifa,"
amesema Dkt. Biteko.
Amesema pia kuwa maendeleo yaliyofikiwa yamepongezwa na
taasisi za kimataifa zikiwemo Benki ya Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC).
Amewataka Wana Bukombe na Tanzania kuhakikisha mwaka mpya
wa 2025 unaenziwa kwa kudumisha upendo, kuvumiliana na kusaidiana ili kila
mmoja kuwa chanzo cha furaha kwa mwenzake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine
Shigella aliishukuru serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe. Dkt. Biteko
kwa jitihada za kuendelea kuwa karibu na wananchi wa Bukombe na Mkoa wa Geita
katika upatikanaji wa maendeleo.
"Pamoja na majukumu yako ya kitaifa, Mheshimiwa
Naibu Waziri Mkuu umeendelea kuwa nasi karibu nasi kuchochea maendeleo ya Mkoa
na Jimbo letu la Bukombe," amesema Shigella.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma
Mwassa amepongeza kwa hatua ya kujumuika na kusherekea pamoja na wananchi na
kusema hatua hiyo inawezesha wananchi kuwa karibu na viongozi wao
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Nicholaus
Kasendamila amewataka wakazi mkoa huo wasifanye makosa kitapofika kipindi cha
uchaguzi.
"Tulishakubaliana kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi
Mkuu na upande wa urais tunaye Rais, Samia, Ubunge na udiwani tusifanye
makosa," amesema Kasendamila.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni