Ofisi ya Msajili wa Hazina yajikita kwenye matumizi ya TEHAMA

 

Katika zama hizi za maendeleo ya kidijitali, ambapo ufanisi wa mashirika unategemea teknolojia, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), chini ya uongozi wa Bwana Nehemiah Mchechu, inaongoza juhudi za kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zake.

Hiyo haiishii hapo, Ofisi ya Msajili wa Hazina inakwenda mbali kwa kutoa wito kwa taasisi za umma, mashirika na wakala wa Serikali kukumbatia kwa kikamilifu matumizi ya TEHAMA ili kuleta tija iliyokusudiwa.

Bwana Mchechu hivi karibuni alisisitiza, “Tumejizatiti kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kazi zetu za msingi ikiwa ni mkakati wa kuongeza uwajibikaji na hivyo kuharakisha michakato mbalimbali katika taasisi za umma.”

Kuimarisha Ufanisi Katika dunia hii ya kisasa, Ofisi ya Msajili wa Hazina inatambua kwamba matumizi ya teknolojia yanaweza kuboresha huduma za umma.

Dhana hii inaungwa mkono na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye aliwahi kunukuliwa akisema, "Teknolojia inabadilisha jinsi tunavyofanya kila kitu huduma za umma zinapaswa kubadilika pia na ili iwe hivyo hatunabudi kukumbatia matumizi ya TEHAMA.”

Maboresho ya kiteknolojia Bw. Mchechu alisema OMH iko kwenye mchakato wa kufanya maboresho makubwa kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuandaa dashibodi ambayo itarahisisha utekelezaji wa majukumu.

“Mashirika ya Umma yanashauriwa kutenga bajeti kwa ajili ya uwekezaji katikaTEHAMA na kuhakikisha mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi,” alisema Bw. Mchechu.

OMH tayari inatumia mifumo mbalimbali inayolenga kutatua mahitaji tofauti ya kiutendaji.

Miongoni mwa mifumo hiyo ni PlanRep ambao ni mahususi kwa ajili ya kuandaa mipango, bajeti na kutoa taarifa ya matumizi kutoka kwenye Mfumo wa MUSE.

Sanjari na mfumo huo ni mfumo wa MUSE kwa ajili ya kufanya malipo, na ule wa OTRMIS (OTR Management Information System) kwa ajili ya kuingiza taarifa kuhusu wajumbe wa Bodi na taarifa za fedha za robo na za mwaka.

Mifumo mingine ni ile ya NeST kwa ajili ya Kufanya Manunuzi; na GAMIS kwa ajili ya kuweka taarifa za mali ( Assets register).

Chapisha Maoni

0 Maoni