Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko ameagiza kufumuliwa kwa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha
Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO) kufuatia kituo hicho kushindwa kuwahudumia wananchi
kwa viwango vinavyotarajiwa.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo leo tarehe 9
Januari, 2025 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea kituo hicho pamoja na
mambo mengine kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa mwezi Aprili,
2024.
Dkt. Biteko ameshangazwa na hatua ya TANESCO
kuweka kando maelekezo ya mwezi Aprili 2024 yaliyolitaka Shirika hilo
kuondokana na matumizi ya namba za kulipia kwenye utoaji wa huduma na kuomba
namba ya bure ya huduma (free toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania -TCRA ili kuwapa unafuu wananchi wanaohitaji huduma za TANESCO.
"Wewe ulishapiga simu, pesa yako
ikakatwa na huduma usiipate? Wananchi wanaumia sana!" naagiza kuundwa upya
kituo ili kuongeza ufanisi na tija kwa Wananchi, "kituo hiki kinategemewa
na Watanzania wengi na huduma inayotolewa hapa hairidhishi kabisa,"
amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Rais Samia imetoa
fedha nyingi kuhudumia kituo hicho lakini utendaji wake ni mbovu kuliko huduma
ya kituo.
TANESCO ilielekezwa kuachana na matumizi ya
namba za kulipia Kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma
(toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania-TCRA ili kuwapa unafuu wa
Wananchi wanapopiga kuhitaji huduma za TANESCO.
Dkt. Biteko ametoa wiki moja kwa uongozi wa
TANESCO kufanya maboresho ya Kituo hicho na matokeo yake yawe wazi kwa Wananchi
kutokana na huduma zake.
Akizungumzia utendaji wa Kituo hicho, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Abubakar Issa amesema kulikuwa na
changamoto za kibajeti. Aidha amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania TCRA watakaa haraka na kuanza matumizi ya namba bila
malipo ili kutoa unafuu kwa wananchi na kuleta tija kwa watumiaji.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishti
0 Maoni