Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa
Ruvuma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 umeidhinishiwa Shilingi bilioni 38.394 kwaajili ya kufanya
matengenezo na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 1145, madaraja madogo
50 na makalavati 57.
Kati ya fedha hizo Sh.bilioni 7.8 bajeti ya barabara kuu,
Sh.bilioni 9.8 zinatokana na tozo ya mafuta, Sh.bilioni 4.5 fedha kutoka mfuko
wa Jimbo na Sh.bilioni 16.2 ni fedha za mradi wa Agri-connect chini ya Umoja wa
Ulaya (EU).
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wa Ruvuma, Mhandisi
Silvester Chinengo wakati akitambulisha barabara mpya ya Muungano-Majengo na
barabara ya Kilimo Mseto-Pm House zenye urefu wa Km 1.5 kwa gharama ya Sh.milioni 949 pamoja na barabara ya
Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa Km 1.1 kwa gharama ya Sh.milioni 426.
“Barabara hizi zimejengwa kutokana na fedha za tozo ya
mafuta na zimeleta mabadiliko makubwa kwenye mitaa kwa sababu wakati wa mvua
wananchi waliathirika na mafuriko pamoja na matope, kwa sasa ni msaada mkubwa
kwa wakazi wa mitaa hiyo na mali zao, pia zitarahisisha sana shughuli za usafiri na usafirishaji kwa
wananchi.”
TARURA mkoa wa
Ruvuma inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Km. 71,146.21,madaraja
306, makalavati 531, drifti 14 na mitaro yenye urefu wa Km. 6.91 ambapo Km.
2312 ni za mjazio, Km. 3873.85 ni za mkusanyo, Km. 959.52 ni za jamii, Km.
128.66 ni lami na zege, Km. 1429 ni changarawe na Km. 5588 ni udongo.
Aidha, aliongeza kuwa, Serikali imetenga Sh.bilioni 2.28
kwaajili ya kuondoa vikwazo barabarani chini ya mradi wa RISE ikiwemo kujenga
madaraja na barabara za changarawe katika Halmashauri ya Madaba, Mbinga Mji,
Halmashauri ya wilaya Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
Denis Timoth mkazi wa mtaa wa Matogoro, ameipongeza
Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mingi ya barabara ili kuwaondolea
wananchi kero ya kusafiri wanapotoka eneo moja kwenda lingine kwaajili ya
shughuli zao za kiuchumi.
Agnes Komba mkazi wa mtaa wa Makambi alisema, ujenzi wa
barabara za lami umewasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa
uchumi wa mtu mmoja mmoja kwani hivi sasa mitaa na maeneo mengi hakuna adha ya
usafiri na usafirishaji.


0 Maoni