Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Hazara Chana amewataka Maafisa
Wanyamapori wote nchini kuchukua hatua madhubuti ya kulinda na kuhifadhi
wanyapori ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kupambana na changamoto za
ujangili.
Mhe. Chana
ameyasema haya leo Desemba 03, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi semina
ya siku mbili inayowahusisha Maafisa Wanyamapori kutoka wilaya 138 hapa nchini.
Amewataka Maafisa
Wanyamapori hao kutoa ushauri kwenye vikao vya Kamati za madiwani zinazoshughulikia
Uchumi na Mazingira kwenye Halimashauri wanazotoka ili kuimarisha uhifadhi.
Amesema Tanzania
ni miongoni mwa nchi nne zinazoongoza duniani kwa kuwa na bioanuai nyingi
kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya
Rais Dkt. Samia.
Amesema
kupitia sekta hiyo kila mwaka imechangia kutoa ajira za moja kwa moja kwa
vijana takriban milioni 1.6 na hivyo kuwataka maafisa wanyapori nchini kufuata
maadili ya kazi zao katika kulinda na kuthamini rasilimali hiyo ikiwemo
kutojihusisha na vitendo vya ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo.
“Nipende
kuwakumbusha kuwa waadilifu na tuzingatie maadili ya utumishi wa umma ikiwa ni
pamoja kutojihusisha na vitendo vya ujangili, rushwa na wizi kwa faida yenu
wenyewe na kwaq faida ya umma uliowaamini kusimamia rasilimalim,” amesisitiza
Mhe. Chana.
Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula amewaomba Maafisa Wanyamapori
wote kuzingatia mafunzo yanayotolewa na Wizara.
Kwa upande
wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili ana Utalii Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba,
amesema Serikali imechukua hatua
mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa wananyamapori ikiwa
ni pamoja na kuandaa sera, kanuni, mikakati na miongozo mbalimbali ya kulinda
rasilimali za Wanyama Pori.
“Wizara
inatambua mchango mkubwa wa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya katika kutekeleza
sera ya wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Wanyamapori Sura ya 283,”
Amesema Kamishna Wakulyamba.
Amesema
Serikali imeweka utaratibu wa kisheria unaowezesha uanzishwaji wa maeneo
Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ili kutambua shughuli za uhifadhi kwenye
maeneo hayo sambamba na kutatua chngamoto zinazowakabili za wanyamapori wakali
na waharibifu katika maeneo yao.
Mkurugenzi
wa Idara ya Wanyamapori Dkt Alexander Lebora amefafanua kuwa katika semina hii
washiriki watafundishwa mfumo wa kielektroniki wa kukusanya taarifa.
Na. Saidi Lufune- Dodoma
0 Maoni