Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeongoza Watanzania na wapandaji wengine zaidi ya
230 kutoka mataifa ya China, Marekani na Ufaransa leo Desemba 05, 2024 kupanda
Mlima Kilimanjaro kupitia Lango la Marangu lililopo mkoani Kilimanjaro.
Watu hao wamepanda
mlima huo kwa lengo la kwenda kupandisha Bendera ya Tanzania ikiwa ni ishara ya
kumbukumbu ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza
kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wiliya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lazaro
Twange, amewaasa wapandaji waliojitokeza kupanda mlima Kilimanjaro kulinda
mazingira ya mlima kwa kupanda miti.
DC Twande
alisema, Tunapopanda miti tutarejesha uoto wa asili, uoto ukirejea barafu
itaongezeka na kusababisha ongezeko la maji yanatiririka katika mabwaya ya
Nyumba ya Mungu, pangani na Lake Chala, kwani chanzo chake ni mlima
Kilimanjaro.
Naye,
Mwenyekitii wa Bodi ya Wadhamini TANAPA (Jenerali Mstaafu) George Waitara
aliwataka wapandaji hao kuwa na uvumilivu na kusaidiana wanapoona mwenzao
amekumbwa na ugonjwa wa mlima.
"Nawaasa
wapandaji wote kufuata maagizo na maelekezo kutoka kwa viongozi wa mlima
(guides), viongozi hawa ni wazoefu wa huu mlima na wanajua dalili zote,
wakiwaambia tembeeni taratibu au kunywa maji fanyeni hivyo, mkifanya hivyo
mtafika kileleni,” aliongeza Jenerali Waitara.
Naye, Naibu
Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana Mwishawa,
alishukuru kundi kubwa la Mabalozi waliojitokeza kupanda mlima na kuongeza kuwa
uwepo wao sio tu ni hamasa kubwa kwa
Watanzania bali pia wataendelea kuwa Mabalozi wazuri wa utalii katika nchi
wanazozisimama hasa hasa kuutangaza mlima kilimanjaro na vivutio vingine
kuvutia watalii wengi zaidi.
Vilevile, Mwakilishi
wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Zara Tours, kampuni aliyopewa dhamna ya
kuwapandisha watu mlimani, Ndugu Bernard Sahini alitumia nafasi hiyo
kuwahakikishia wapandaji wote usalama wa hali ya juu na huduma nzuri Kwani
wamejiandaa vyema na watafanya kazi kwa weledi uliotukuka.
Hafla iyo ya
kupandisha watu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 63 ya
Uhuru wa Tanganyika kupitia kampeni ya TWENZETU KILELENI imehudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa serikali, ikiweno Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro,
Mabalozi kutoka nchi mbalimbali,Jeshi la Wananchi (JWTZ), Bodi ya Wadhamini
TANAPA,kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na viongozi mbalimbali wa
dini.
Na.
Happiness Sam- Kilimanjaro
0 Maoni