Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema
kuwa Daisle Simion Ulomi, aliyekuwa ameripotiwa kwamba amepotea, alifariki
dunia baada ya kupata ajali mbaya na pikipiki aliyokuwa akiitumia siku ya
Desemba 11, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 16, 2024 na Kamanda wa
Polisi wa Kanda hiyo SACP Jumanne Muliro ambapo ameeleza kuwa tarehe 11
Desemba, 2024 Jeshi hilo lilipata taarifa ya kupotea kwake na ndugu hawakuwa
wanampata kwenye mawasiliano ya simu, baada ya yeye kuondoka ofisini kwake
Sinza na kudai anaelekea Temeke kufuatilia makontena yake ya biashara.
SACP Muliro amesema Ulomi aliondoka eneo lake huku
akitumia pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe, ufuatiliaji
umefanyika kwa kushirikiana na ndugu na kubainika kuwa Ulomi alipelekwa kituo
cha afya cha Makuburi Ubungo External mchana wa tarehe 11 Desemba, 2024 baada
ya kupata ajali mbaya na pikipiki aliyokuwa akiitumia, wasamaria wema
walimsadia kumpeleka kwenye kituo hicho akiwa hajitambui na hakuwa na
kitambulisho chochote.
Awali, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala,
Lydia Nzema akizungumza na waandishi wa habari amesema walipokea mwili wa Ulomi
Desemba 11, 2024 ukitokea Zahanati ya Makuburi, ikidaiwa kifo chake kimetokana
na ajali.
“Hii ikiwa na maaana kama kituo cha afya alichopelekwa
kwa matibabu ilikuwa ni zahanati ya Makuburi, sisi tumepokea kutoka zahanati
hiyo mwili ambao haujatambuliwa na tulihifadhi chumba cha maiti kama ilivyo kwa
miili mingine,” amesema Nzema.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Mwananyamala Dk Zavery Benela amesema mwili wa Ulomi ulifikishwa hospitalini
hapo na kuhifadhiwa kwenye chumba cha maiti Desemba 11, 2024.
0 Maoni