Tarehe 15 Desemba 2024 Kreta ya Ngorongoro ilipambwa na
tukio adhimu na la kihistoria la maharusi wa Kitanzania kufunga ndoa ndani ya
Hifadhi huku hao wakipunga upepo mwanana kwenye mazingira asilia yaliyozungukwa
na wanyama mbalimbali wakiwemo Big 5.
Bw. Kelvin Mwakaleke na mkewe Jackline Nyalu wamefunga
Ndoa ndani ya Kreta ya Ngorongoro wakisindikizwa na wazazi, ndugu, jamaa na
marafiki huku wakishuhudiwa na macho ya Wanyama mbalimbali wakiwemo Simba,
Faru, Tembo, Nyati, Chui, Pundamilia, Nyumbu, Thomson Gazelle, ambao wamekuwa
mashuhuda wa tukio hilo lililofanyika
pembeni mwa bwawa maarufu la Ngoitoktok wakati huo Viboko wakinogesha shughuli kwa kuogelea.
Akielezea tukio hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Uhifadhi Mariam Kobelo anayesimamia huduma za Utalii na Masoko NCAA ameeleza
kuwa "Leo ni siku ya furaha na ya
kipekee isiyosahaulika, tumeshuhudia tukio adhimu na akramu lenye baraka
za Mungu kwa maharusi hawa kufunga ndoa kwenye bustani ya Eden (Ngorongoro
Crater).
Hili ni jambo jipya na la kwanza katika historia ya NCA
na limechagizwa na juhudi za Utangazaji wa vivutio vya utalii vinavyopatikana
ndani ya NCA huku vimeendelea kuibua chachu kwa watanzania wengi, ndio maana
unaona leo tumeona zao jipya la utalii. Tunaendelea kuwakaribisha wananchi
wengine kuja hifadhi ya Ngorongoro kwa matukio kama haya" alifafanua
Kamishna Kobelo.
Kufunga ndoa ndani ya hifadhi ni fursa muhimu katika
kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro hali inayoamsha ari kwa
watalii wa ndani kuongezeka na kuchangia mapato ya Serikali.
Akielezea tukio hilo huku akiwa na nuru ya tabasamu na
fursa Bwana harusi Kelvin Mwakaleke akiwa na mkewe Jackline ameeleza kuwa
kufunga ndoa ndani ya hifadhi ilikiwa ndoto yake ambayo hatimae imetimia.
"Nilimuomba Mungu kuniongoza kufanikisha tukio hili,
kufunga ndoa kreta ni uzoefu ambao siwezi kuusahau, ni eneo lenye vivutio vya
kila aina kwa mtu yoyote kutembelea, lina uzuri wa asili wanyama wengi na uoto
wa asili uliohifadhiwa vema, mimi, mke
wangu na ndugu wachache tuliounganika hapa tutakuwa mabalozi wa kuitangaza
hifadhi ya Ngorongoro" alisema Bw. Mwakaleke.
Aidha, alishukuru kwa huduma nzuri iliyotolewa na wahifadhi wote waliokuwa bega kwa bega kuhakikisha wanakuwa salama na kufurahia mandhari na kukamilisha ndoa yao.
Na. Kassim Nyaki- Ngorongoro Kreta
0 Maoni