Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali haipendi
kusikia na haitavumilia kusikia uwepo wa vitendo vya unyanyasaji kwa watu wenye
ulemavu na wale watakaojihusisha na vitendo hivyo itawachukulia hatua
kikamilifu.
DKt. Biteko
amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa katika maadhimisho ya Siku ya watu wenye ulemavu iliyofanyika sambamba
na uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu wenye Ualbino na
Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi kwa wenye ulemavu.
“Hatuwezi
kuvumilia kuona watu wanaojihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa watu wenye
ulemavu, eti wananauza viungo vya albino, au wanafanya mauaji, nawahakikishia
tutakula nao Sahani moja!,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema
Kauli mbiu ya mwaka huu: ‘Kukuza uongozi kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya
mustakabali Jumuishi na endelevu ni muafaka kwa vile inaendana na tamko la
kimataifa la kukuza ufahamu wa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu duniani.
Dkt. Biteko
ameongeza kuwa Serikali imeweka miongozo mbalimbali ikiwemo kutenga fedha kwa
ajili ya makundi maalum ikiwemo watu wenye ulemavu.
“Kitengo cha
Ufuatiliaji na tathimini kiko ndani ya Ofisi hii ya Waziri Mkuu, kifanye
ufuatiliaji kujua Ofisi na halmashauri zinavyotenga fedha kwa ajili ya makundi
maalum na tupate taarifa ya ufuatiliaji wake,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amesema
haipendezi kuona tunakubaliana na kuweka maazimio ya kazi lakini utekelezaji
wake unabaki katika makablasha.
Aidha,
amewaelekeza Wakuu wa wote wa Mikoa nchini kutekeleza mpango kazi wa haki na
ustawi kwa watu wenye ualbino na kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu,
kuhakikisha kila halmashauri nchini inatenga bajeti ya ununuzi wa Vifaa saidizi
kwa kuzingatia uhitaji na viwango vya ubora wa Vifaa hivyo na Wizara za kisetka
kutekeleza Mpango na mkakati huo kwa mujibu uliowekwa na Ofisi ya Rais,
TAMISEMI.
Kwa upande
wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu,
Mhe. Ridhiwan Kikwete, amesema Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha jamii
inatambua haki za kijamii kwa watu wenye ulemavu na ndiyo msingi wa kuzinduliwa
kwa mkakati huo.
Naye Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mhe. Riziki Lulida amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za
kuwawezesha nakuwakomboa watu wenye ulemavu kwa maendeleo endelevu na jumuishi.
“Katika
kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia walemavu wanaunga mkutano
jitihada za matumizi ya nishati safi pamoja na kushiriki katika shughuli
mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa madini katika migodi,” amesema na kuongeza kuwa
wanazidi kumuunga mkono Rais ili atekeleze maono yake.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HelpAge Tanzania, Smart Daniel amesema kila binadamu anavyo vigezo
vya kuwa mlemavu maishani kwa kuzaliwa, kupata ajali au kuzeeka na baadhi ya
viongo kushindwa kufanya kazi kawaida.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati



0 Maoni