WAZIRI MKUU,
Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Afrika
Mashariki kuendelea kujadili changamoto katika utoaji haki na kuweka mipango
endelevu ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo kupitia mikutano yake.
Mhe. Majaliwa
ametoa wito huo leo (Disemba 03, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika mkutano wa Ishirini na Moja wa chama hicho uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa hotel ya GranMelia jijini Arusha.
“Mkutano huu
pamoja na mambo mengine ni muhimu kujadili masuala muhimu ya Kitaifa na Kikanda
katika mfumo wa utoaji haki, pia nina imani kupitia mkutano huu mtajadili
umuhimu wa kuimarisha na kuboresha mifumo ya utoaji haki na kutumia ukuaji wa
teknolojia ili kuboresha kwenye ufanisi wa majukumu yenu,” alisema Mhe. Majaliwa
.
Pia, Mhe.
Majaliwa amewataka Majaji na Mahakimu hao kujadili namna mifumo ya utoaji haki
inavyoweza kuwa chachu ya ushirikiano wa kikanda na ukuaji wa uchumi. “Mnapaswa
kujadili namna mifumo ya utoaji haki inavyoweza kusaidia katika kukuza
mtangamano wa kikanda na ukuaji wa uchumi.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya maboresho na mapitio ya mifumo
ya utoaji haki yenye lengo la kuimarisha ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
“Serikali
yetu, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, tumefanya maamuzi
muhimu ya kisera kijamii na kiuchumi ambayo yanaakisi mwelekeo wetu wa
maendeleo wenye lengo la kuboresha ustawi na ustawi wa watu wa Tanzania,”
alisema Mhe. Majaliwa.
Kadhalika
Mhe. Majaliwa amesema kuwa Kupitia Mpango ya Maendeleo ya Miaka Mitano,
Serikali ya Tanzania imedhihirisha dhamira yake ya kuboresha mfumo wa utoaji
haki. Mnamo 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliteua "Tume ya
Rais ya Haki Jinai" yenye lengo la kuleta mageuzi katika mfumo wa haki za
jinai.
Naye Waziri
wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa Serikali inatahamini
kazi kubwa zinazofanywa na Mahakimu na Majaji kwa kuwa wao ni kitovu cha amani
na utulivu.
Kwa upande
wake Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amesema kuwa kupitia mkutano huo watapata
nafasi ya kujifunza na kubalishana uzoefu. “Tumeweza kubadilishana uzoefu
katika mifumo ya haki jinai na namna tunavyoweza kuitumia teknolojia katika
kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa ufanisi na haraka
bila ucheleweshaji.”


0 Maoni