Serikali
imesema itaendeleza jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kufanya
biashara kwa lengo la kuboresha shughuli za biashara, uwekezaji na kukuza
uchumi wa nchi.
Sambamba na
kushirikiana na sekta binafsi ili kutatua changamoto zinazowakabili
wafanyabiashara nchini ikiwa ni pamoja kujenga na kuimarisha miundombinu kwa
ajili ya usafiri na usafirishaji.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo
Desemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Majadiliano
ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi Mwaka 2024 na
Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo
Tanzania (TCCIA).
Dkt. Biteko
ameeleza umuhimu wa sekta binafsi na kusema kuwa nchini Tanzania na Afrika kwa
ujumla inakisiwa kuwa vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira
wanategemea sekta binafsi ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na
kutatua changamoto za sekta binafsi.
“Hivi
karibuni mlitoa malalamiko kadhaa ikiwemo ya kukwamisha shughuli za biashara na
Serikali imeyatatua kwa kushirikiana nanyi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka
ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja
baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji
biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanywa marekebisho ya sheria na kanuni 55
na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi.
Amesisitiza
“Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka mfano sasa tuna
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia,
imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka
siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es salaam hadi Tunduma.”
Pamoja na
hayo Dkt. Biteko amefafanua kuwa Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA)
imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza mapato
kiasi cha shilingi bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais
Samia za kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Fauka ya
hayo, amezungumzia viashiria vya ukuaji wa uchumi na kusema kuwa kumekuwepo na
ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme ambapo awali hayakuwahi kuzidi
megawati 219 kwa mwaka na kuwa mwaka 2024 mahitaji ni megawati 420.
“Mkifanyabiashara
maana yake mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka na hii ni kwa sababu
viwanda vingi vimejengwa na uchumi unachangamka. Tunaanza kuona wananchi
wanatumia umeme megawati 52 na viwanda vinatumia megawati 48 hii ni kiashiria
kuwa uchumi unaendelea kukua vizuri,” amebainisha Dkt. Biteko.
Vilevile,
amewaasa wafanyabiashara nchini kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze
kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali itakayosaidia utoaji huduma za kijamii
kwa wananchi na kuchochea maendeleo huku akiwataka kuzalisha malighafi na
bidhaa zenye ubora zitakazovutia masoko na kutoa ajira kwa watu.
“Nchi yetu
tutaijenga wenyewe na tuambiane ukweli kwamba kulipa kodi ni wajibu wetu, kwa
mikataba hii iliyowekwa saini hapa leo TCCIA muwe mawakala wa kutoa elimu ya
mlipa kodi kwa wananchi ili watu waone heshima ya kulipa kodi,” amesema Dkt.
Biteko.
Ameendelea
kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza
nchini huku akivitaka vyama vya kisekta kuepuka migogoro na kusisitiza upendo,
ushirikiano na mshikamano miongoni mwao.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. John Lukuvi amesema
kusanyiko hilo la zaidi ya wafanyabiashara na wakulima 300 kutoka nchi nzima ni
muhimu na kuwa kupitia jukwaa hilo Serikali itaendelea kushirikiana nao ili
kukuza sekta binafsi nchini.
Mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe.
Edward Mpogolo amesema kuwa Mkoa huo umekuwa na ushirikiano mzuri na TCCIA
katika shughuli mbalimbali.
“Wafanyabiashara
hawa wamekuwa wakipongeza jitihada za Rais Samia kwa kupunguza msongamano wa
meli bandarini, kuboreshwa kwa miundombinu wezeshi ya viwanda mfano zaidi ya
shilingi trilioni moja imetolewa katika miradi ya barabara ya DMDP na sasa
umeme uko wa kutosha na wanaendelea kufanya biashara vizuri,” amesema Mpogolo.
Rais wa
Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja kwa niaba
ya wafanyabiashara nchini amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuifungua
nchi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania na hivyo kusaidia
biashara kufanyika kwa utulivu.
Amesema
taasisi yake ina ofisi katika nchi za China, Uturuki na Uingereza na hivyo
inarahisisha kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na nchi mbalimbali.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kurahisisha maendeleo ya biashara katika Bandari ya Dar es salaam
sasa meli zikija na mizigo zinapakuwa ndani ya siku chache, pia tunamshuru Rais
Samia kwa kuunda tume ya kushughulikia masuala ya kodi,” amesema Minja.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar
Kissanga amesema kuwa taasisi yake inalenga kuunganisha wadau wa biashara na
kukuza sekta ya biashara na kilimo nchini.
“Katika
kipindi cha miaka 36 TCCIA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili
kuimarisha ushindani na kuvutia wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema
Kissanga.
Ameongeza
kuwa lengo TCCIA ni kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika
kuleta maendeleo endeleo na kujenga uchumi imara huku akimpongeza Rais Samia
kwa jitihada zake za kuhakikisha kunakuwepo na ushiriki wa sekta binafsi katika
kukuza uchumi wa nchi.
Kissanga
ametaja baadhi ya utekelezaji wa shughuli za TCCIA katika kipindi cha mwaka
2024 kuwa kutoa mafunzo ya kuelimisha Watanzania kuhusu Soko Huru la Afrika
kutoka katika mikoa nane, imesafirisha shehena za bidhaa mbalimbali katani
ikiwa ni asilimia 70 ya shehena yote.
Vilevile,
imefanya ukaguzi wa viwanda 37, na kufanya Jukwaa la Biashara ya Korosho
Tanzania na kuleta nchini zaidi ya kampuni 100. Sambamba na kuzisaidia kampuni
za Tanzania kupata fursa za uwekezaji na masoko kutoka nchi mbalimbali duniani.
Mkurugenzi
Mkazi wa Kampuni ya Trademark Afrika, Elibariki Shammy amesema taasisi yake
inalenga kuisaidia Watanzania na Afrika kwa ujumla ili iweze kufanyabiashara na
dunia na kuwa ina wadau kutoka sekta ya umma na binafsi na hivyo wanashukuru
kwa kuendelea kuaminiwa katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha,
kupitia Kongamano hilo Dkt. Biteko ameshuhudia utiaji saini wa baadhi ya
mkataba ikiwemo mkataba kuwezesha kufanya kazi pamoja kati ya Serikali na sekta
binafsi, ushirikiano wa biashara kati ya TCCIA na Chuo Cha Biashara (CBE)
ambapo CBE inatarajia kuwa na mitaala ya biashara ya wanagenzi na hivyo
ushirikiano huo utasaidia kufikia wafanyabiashara watakaosaidia kufundisha
wanafunzi.
Mkataba mwingine
uliowekwa saini ni wa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha
wanachama wa TCCIA kulipa kodi kwa hiari kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na kurahisisha ulipaji kodi na kutoa elimu ya namna kiwango na muda wa kulipa
kodi.
Kongamano
hilo limeongozwa na kaulimbiu “Kuongeza Ufanisi wa Majadiliano na Ushindani wa
Mauzo ya Nje kwa Ustawi wa Uchumi” limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na
Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, viongozi mbalimbali pamoja na
wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Na Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni