Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewaasa wahitimu wa Chuo
cha Taifa cha Utalii (NCT) kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma bora kwa
watalii ili kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya watalii nchini ambapo hadi
kufikia mwezi Oktoba 2024, idadi ya watalii imefikia asilimia 96% (1,750,198).
Ameyasema
hayo leo katika Mahafali ya 22 ya Chuo cha Taifa cha Utalii yaliyofanyika
kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 595 katika ngazi za Astashahada na Stashahada
katika Fani za Ukarimu, Utalii na Uratibu wa Matukio kwa mwaka 2023/2024.
‘’Nchi yetu
imeendelea kupokea wageni wengi ambapo ni matunda ya juhudi kubwa za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza
utalii kupitia filamu za "Tanzania The Royal Tour na "Amazing
Tanzania " pamoja na uongozi bora.Hivyo ninyi ambao mmepikwa katika Chuo
bora cha Utalii na Ukarimu nchini nategemea mkalete mageuzi katika huduma
mtakazotoa kwa watalii na wageni kwa ujumla, ili watalii wanaotembelea nchini
wapate huduma kulingana na thamani ya fedha yao na pia washawishike kurejea
nchini na kuitangaza Tanzania kwa ndugu na jamaa zao” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha,
amewapongeza wahitimu hao na kuwaasa kutumia vyema ujuzi walioupata ili kuziba
pengo la malalamiko katika eneo la utoaji wa huduma bora kwa wageni.
Katika hatua
nyingine, Mhe. Chana amekipongeza Chuo cha Taifa cha Utalii kwa kufundisha
lugha ya kichina na kijerumani
itakayosaidia kuliteka soko la China na Ujerumani kwa kujiweka tayari
kupokea wageni kutoka nchi hizo.
Naye, Mkuu
wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey aliwapongeza na kuwataka
wahitimu hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu huku wakiwa na kiu kubwa ya
kuleta maendeleo kwa Taifa.
"Nawapongeza
kwa kutumiza vigezo tunaamimi tumewaandaa vya kutosha kwa ajili ya watanzania
na kuendeleza mabadiliko ndani na nje ya nchi," alisema Dkt.Mtey.
Na. Happiness Shayo - Dar es Salaam
0 Maoni