Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mhandisi Victor Seff
amewataka Mameneja wa TARURA wa Mikoa na Wilaya zote nchini kufanya ukaguzi na
matengenezo ya Miundombinu ya barabara
zinazosimamiwa na TARURA mara kwa mara ili kubaini kasoro na kuchukua hatua za
haraka kuondoa kasoro hizo.
Kauli hiyo
ameitoa wakati alipofanya kikao kazi na Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa TARURA
katika Ukumbi wa Odotorium, Millennium Tower - Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Mhandisi
Seff ameonesha kutofurahishwa na hali ya matengenezo ya Miundombinu ya Barabara
zinazosimamiwa na TARURA kufuatia ziara yake ya hivi karibuni aliyoifanya
katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
"Suala
la matengenezo ya Miundombinu ya Barabara bado hatujafanya vizuri sana. Ukiona
maeneo mengi bado hayafanyiwi matengenezo kwa wakati na haswa upande wa
madaraja na mifereji ambayo tukikutwa na mvua yanaweza kutokea majanga ikiwemo
miundombinu ya barabara kukatika na hata kupelekea maeneo mengine kutofikika
kabisa.”
"Kwa
hiyo leo tunakumbushana kuhusiana na hilo ili tuwe makini kuanzia kwenye
upangaji (planning) mpaka kwenye utekelezaji ili kuhakikisha kwamba tunafanya
matengenezo kwa wakati kuzuia barabara kukatika hata yale maeneo ambayo
tungeweza kuyaokoa kabla mvua hazijaanza kunyesha," amefafanua Mhandisi
Seff.
Mhandisi
Seff aliwaasa Mameneja hao kuwa na utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara kwenye miundombinu ya barabara na kama watagundua kasoro wanapaswa kuandaa
taarifa na kuiwasilisha Makao Makuu ili hatua za haraka za marekebisho ya
kasoro hizo ziweze kuchukuliwa.
"Shida
sio mvua ila shida ni je tunafanya kazi zetu kama tunavyotakiwa?"
"Tusisubiri
mpaka madaraja yavunjike ndio tunakimbilia kuomba hela za dharura. Tutimize
kwanza jukumu letu halafu kama ikitokea mvua ni nyingi kweli na sio tunasingizia
mvua zilikuwa kubwa kumbe sisi wenyewe hatukufanya matengenezo yaliyopaswa kwa
wakati muafaka."
Amesema
suala la matengenezo ya Miundombinu ya barabara lazima tulipe umuhimu wa hali
ya juu kabisa haswa kwa madaraja na barabara mpya ambazo zimejengwa ili tuweze
kutambua muda ambao umesanifiwa uweze kufikiwa kama ubunifu (designing)
inavyosema.
Naye,
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala Bi. Azimina Mbilinyi aliwashukuru
Mameneja hao kwa kazi wanazoendelea kuzifanya pamoja na changamoto nyingi wanazokabiliana
nazo na kuwaasa kuendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba
wanabaki katika mstari.



0 Maoni