Kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha mto Trippi kilichopo Kijiji cha Trippi Kata ya Gehandu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu umeweza kupunguza utoro kwa asilimia 98 na kuongeza ufaulu wa mtihani wa darasa la saba kwa asilimia 91 kwa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Trippi.
Hayo
yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Trippi Mwl. Adwee Hesiali ambapo
amesema kabla ya kivuko hicho wanafunzi wanaoishi upande wa pili walikuwa
wakikosa masomo kwa takriban miezi minne na kipindi cha masika ilifika hadi
asilimia 51.
“Wananchi
walijitahidi kujenga kivuko cha miti lakini kilisombwa na maji kwenye mto huu,
lakini kukamilika kwake kimeweza kuongeza ufaulu kutoka asilimia 84 mwaka jana
hadi kufikia asilimia 91 mwaka huu.
“Kwa kweli
kitaaluma tumepanda na utoro umekwisha, hii ni kutokana na ujenzi wa kivuko
hiki kwani imetuondolea adha kwa wanafunzi wetu”.
Mwl. Hesiali
amesema kuwa wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwezesha kivuko hiko na kuongeza kusema kwamba kwa sasa wapo
vizuri.
Naye, Diwani
wa Kata ya Gehando Mhe. Alex Tango ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa
kuwajengea kivuko katika mto Trippi “Kivuko hiki kimekuwa mkombozi kwa
wanafunzi ambao walishindwa kuhudhuria masomo katika kipindi chote cha
masika".
Amesema
kivuko hicho imesaidia pia kuinua uchumi wa wananchi kwa upande wa pili kwani
kuna wakulima wa mbaazi ambao walikuwa wanavusha mizigo kwa kichwa ila kwa sasa hawana shida
tena na kusema msimu ujao wanatarajia kivuko hicho kitasaidia sana kuinua
kipato cha wananchi wake.
Mhe. Tango
alisema licha ya ujenzi wa kivuko hiko, TARURA hivi sasa kuna kazi ya ujenzi wa
barabara ya Kainamu-Hasama- Tsawa yenye urefu wa Km. 10 ambapo ujenzi wake
utagharimu shilingi milioni 700 ambapo kukamilika kwake kutasaidia wakazi zaidi
ya 14,000.
“Kwakweli
mimi kama mwakilishi wa wananchi naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa hii
wanayoifanya kilomita hizi za barabara zikikamilika wananchi watakuwa wamepata
mawasiliano na hivyo kujenga imani na Serikali yetu”.
Amesema
wameweka mkakati wa kutunza kivuko hicho kwa kuzungumza na viongozi wa Kijiji
na Kata na hivyo kuweka utaratibu wa kuvusha mizigo mikubwa kwa kuweka ulinzi
ambao utasaidia kulinda wizi wa vyuma.
Kwa upande
wake Bw.Silini Esumale mkazi wa kijiji cha Tsawa ameishukuru Serikali kwa
kuwajengea kivuko cha utalii kwani miaka yote watoto wao hawakuwa wakipata
masomo pia wakazi wengi walikuwa wakipata matatizo mengi, lakini kilio chao cha
muda mrefu Serikali imekisikia na sasa wanapita bila wasiwasi.
Meneja wa
TARURA Wilaya ya Mbulu Mhandisi Nuru Hondo amesema kwamba katika Halmashauri ya
Mji wa Mbulu na Halmashauri ya wilaya wameweza kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais
kwa kujenga barabara ya lami yenye urefu wa Km. 11.2 katika Mji wa Mbulu
(4.2),Mji wa Dongubesh (2.5) na Mji wa Haydom (4.4).
Amesema
katika kipindi cha miaka mitatu bajeti ya wilaya imeweza kuongezeka kwa
42.1% hadi kufikia shilingi bilioni 7.59
kwa mwaka 2023/2024 ukilinganisha na shilingi bilioni 4.41 mwaka 2021/2022,
ambapo wameweza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo madaraja 22 (Mbulu),
madaraja 17 (Mbulu Mji) na hivyo kuweza kuhudumia mtandao wa barabara
wa Km. 1,500.459.



0 Maoni