Wasanii
wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao wakati wa kambi maalumu ya
uchunguzi na matibabu ya moyo itakayofanyika hivi karibuni katika Kliniki ya
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe.
Rai hiyo
imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo itakayotolewa kwa
wasanii.
Dkt. Kisenge
alisema kutokana na tatizo la magonjwa ya moyo kuwa kubwa Taasisi hiyo imeona
ishirikiane na wasanii katika kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kupima magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Katika
kufanikisha hili kutakuwa na zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo
kwa wasanii katika kliniki yetu ya Kawe kwa mwezi wa huu wa Desemba na Januari
2024 kila siku za Jumamosi na Jumapili.”
“Baada ya
kumalizika kwa zoezi hili kutakuwa na utaratibu maalumu kwa wasanii ambao
hawana bima za afya watakaokuja kutibiwa katika kliniki yetu watapata punguzo
la gharama za matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande
wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana
aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuona umuhimu wa kupima
afya za mioyo ya wasanii na kuwapa elimu ya jinsi ya kujiepusha na magonjwa
hayo bila ya gharama zozote zile.
“BASATA
tutasimamia zoezi hili la upimaji kwa wasanii wetu ili kila mmoja anufaike na
upimaji huu kama mlivyosikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo ni kubwa
hivyo basi ni muhimu mkachukuwa hatua za kupima mapema kabla ya kusubiri kuugua,”
alisisitiza Dkt. Mapana.
Naye Kaimu
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga alisema upimaji huo
ni wa muhimu kwani utawapa hamasa wasanii ya kupima mioyo yao na kuchukuwa
hatua baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo.
“Ninawasihi
mtumie vizuri fursa hii kwa kupima mioyo yenu na kupata elimu ya jinsi ya
kujiepuka na magonjwa haya pia elimu mtakayoipata muitumie kuielimisha jamii
inayowazunguka kwani uwezo wa kufanya hivyo mnao,” alisema Dkt. Gervas.

0 Maoni