Wateja wa
hadhi, wastaafu na wafanyakazi wanaopitisha mishahara yao katika benki ya CRDB
kupata punguzo la asilimia 50 wanapohitaji kupata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano kati
ya JKCI na Benki ya CRDB kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao na kutoa
huduma kwa jamii.
Dkt. Kisenge
alisema Benki ya CRDB ni moja ya Taasisi za fedha kubwa nchini inayochangia
maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya hasa kwa
watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
Benki ya
CRDB ni moja ya wadau wa kwanza ambao walitambua umuhimu wa kuwekeza katika
afya hususan matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto ambao wengi wao wanatoka
katika familia ambazo hazina uwezo wa kulipia gharama za matibabu ya moyo,” alisema
Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge
alisema tangu mwaka 2017 Benki ya CRDB imechangia kiasi cha shilingi milioni
775 ambazo zimetumika kulipia upasuaji wa moyo kwa watoto 193.
Kwa upande
wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bruce Mwile alisema makubaliano
waliyoingia na JKCI ni mwanzo wa ushirikiano utakaoleta manufaa kwa wengi
katika maeneo ya huduma za matibabu ya moyo kwa kuwawezesha wateja wa CRDB
kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
“Ushirikiano
wa JKCI na Benki ya CRDB ni mfano mwingine unaoonyesha jinsi tunavyoendelea
kujidhatiti kuhakikisha si tu tunawawezesha wateja wetu kutimiza malengo yao ya
fedha bali pia mwenendo wao katika kutunza afya zao,” Mwile.
Mwile
alisema lengo la ushirikiano huo ni pamoja na kuisaidia jamii ya watanzania
kupata huduma bora za afya na kwa urahisi itakayowasaidia kuweza kujenga uchumi
imara wa nchi.
“Afya ni
nguzo muhimu ya kimaendeleo na kijamii kwani bila afya bora tunakosa nguvu na
uwezo wa kufikia malengo yetu ya kiuchumi na kijamii,” alisema Mwile.
Aidha. Mwile
alisema JKCI imekuwa mnufaika wa muda wote kupitia mbio za CRDB kwani
kinachopatikana katika mbio hizo kiasi kikubwa hupelekwa JKCI kwaajili ya
kuwatibu watoto 100 kila mwaka.
0 Maoni