Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema viongozi wake wakuu akiwemo
Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, ambao walikuwa wanashikiliwa na polisi mkoni
Songwe wameachiwa huru bila masharti jana usiku.
Mkurugenzi
wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA John Mrema amesema hata
hivyo mwanachama wao Mdude hajaachiwa, “RPC kasema wana mahojiano naye pamoja
na mtu mmoja ambaye aliumizwa vibaya na polisi, tunaendelea kufuatilia hali ya
afya yake.”
Jeshi la
Polisi Mkoani Songwe jana November 22,2024 lilitoa taarifa kuwa linawashikilia
Wanachama wa CHADEMA ambao ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe, Joseph
Mbilinyi (Sugu) Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Pascal Yohana Haonga,
Mbunge Mstaafu CHADEMA Mbozi Mlowo, Mdude Mpaluka Nyagali, Apolinary Boniface
Margwe, Afisa Habari CHADEMA na Adam Hassan Kasekwa, Mlinzi wa Mwenyekiti wa
CHADEMA.
Wengine
waliokamatwa ni Paul Joseph Paul, Afisa wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Mbeya,
Kelvin Keneth Ndabila, Afisa habari Kanda ya Nyasa, Mkazi wa Mbeya, Michael
Laison Msongole, Mwenyekiti CHADEMA Wilaya ya Mbozi, Mlowo, Mohamed Abdilah
Ling wanya, Mlinzi wa Mbowe Mkazi wa Dar es salaam, Alfan Hassan Mbire, Mlinzi
wa Mbowe na Ezekia Elia Zambi, Mwenyekiti ACT Wazalendo Mkoa wa Songwe.
Viongozi hao
walikamatwa eneo la stendi ya zamani ya Mlowo Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe
Novemba 22, 2024 majira ya 10:30 asubuhi baada ya CHADEMA kwenda kufanya
mkutano wa kampeni eneo ambalo hawakupangiwa.
Polisi
wameeleza kuwa askari waliwapa amri ya kutawanyika lakini walikaidi ndipo polisi
walipowatawanya kwa nguvu nao wakaanza kwaurushia mawe polisi na kuwajeruhi askari
wawili maeneo ya kichwani, usoni na puani na kwa sasa wanaendela na matibabu
Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.
0 Maoni