Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka
wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kuendelea kuwa viongozi wa mabadiliko katika
soko la ajira la Tanzania, wakienda sambamba na kasi ya dunia katika maeneo ya
ujasiriamali na ubunifu.
Akizungumza
katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu
ya Morogoro, Balozi Nchimbi amesema ni muhimu kwa vyuo vya elimu ya juu na
wahitimu wake kuzingatia kasi ya mabadiliko ya dunia katika maeneo ya ubunifu,
ujasiriamali, na uongozi ili kuleta mapinduzi makubwa katika kutengeneza fursa
za ajira nchini.
Kupitia
mkutano wa baraza hilo uliofanyika leo tarehe 23 Novemba 2024, ukiwa na kauli
mbiu isemayo “Kuwawezesha wanafunzi kufanya mapinduzi katika soko la ajira na
kuchochea upeo mpya wa fursa za kazi,” Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa
mapinduzi hayo, mbali ya kusaidia kutengeneza fursa za ajira, kujiajiri na
kuajiriwa, pia yatakuwa sehemu ya misingi ya kuongeza kasi ya maendeleo ya
kiuchumi nchini.
“Maendeleo
ya teknolojia, masuala ya akili bandia, na uchumi wa kijani vimekuwa vichocheo
vikubwa vya mabadiliko duniani. Sisi Watanzania, kipekee wahitimu wetu,
wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa ufanisi. Ninatoa wito kuhusu
umuhimu wa kutambua umuhimu wa ubunifu katika kutatua changamoto, kwa
kuzingatia maslahi ya taifa,” amesema Balozi Nchimbi.
Alisema kuwa
dunia inabadilika haraka, hivyo ni muhimu kwa wahitimu kuchukua fursa hizo ili
kuleta maendeleo endelevu, huku akiwasisitiza kutumia elimu waliyoipata chuoni
hapo, kuwa sehemu ya kutafuta njia za kuboresha masoko ya ajira kupitia
matumizi ya teknolojia na ubunifu, na kushiriki kwa dhati katika mchakato wa
maendeleo.
Katika
hotuba yake, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa Serikali ya CCM, chini ya uongozi
wa Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya
kutengeneza fursa za ajira na maendeleo ya vijana, kwa sababu kundi hilo ni
nguzo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Aidha, alisisitiza kuwa sekta ya ujasiriamali, ni mojawapo ya sekta zitakazosaidia kufungua fursa za ajira na kukuza viwanda na biashara mpya nchini. Aliwahimiza wahitimu kuwa na mtazamo wa kimataifa na kuona changamoto kama fursa za ubunifu na maendeleo.
Balozi
Nchimbi pia alizungumza kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika maendeleo ya
taifa. Alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume
wanapata fursa sawa katika sekta zote, na aliwahimiza wahitimu wa kike na wa
kiume kujitahidi kutimiza malengo yao kwa usawa na kushirikiana kwa pamoja
katika kuleta maendeleo.
Balozi
Nchimbi pia alitoa wito kuhusu umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wahitimu,
wakijifunza kwa watangulizi wao, hasa katika kuunda mitandao ya kijamii
itakayosaidia kubadilishana uzoefu na kuendelea kujifunza masuala mapya,
ikiwemo mbinu za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
0 Maoni