Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza
wananchi wa Chato kuchagua wagombea wa CCM ili kuendeleza miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika wilaya yao.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Novemba 23, 2024 wakati akihutubia katika Kampeni
zinazoendelea za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Chato
zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Bwanga, vilivyopo mkoani
Geita.
Amesema CCM
ina nia ya kuendelea kuleta maendeleo huku akivitaka vyama vingine vishindane
kwa hoja sio kwa matusi na kuwa nyenzo za kuunganisha Watanzania sio kuwagawa.
“Nawaomba
muwasikilize vyama vingine lakini msifanye kosa la kuwachagua maana wanataka
vyeo tu, msikubali watu wanaowaambia mkunje ngumi hawana ilani iliyopitishwa na
wananchi wala bajeti wanataka muwachague wakafanye kazi gani?,” amehoji Dkt.
Biteko.
Ameendelea
kusema Uchaguzi wa Mwaka 2024, CCM
imejipanga kushinda na si kubahatisha kwa kuwa na mipango yake imeanza kwa
wanachama wake kujitokeza kwenye uandikishaji daftari la wapiga kura kwenye
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“ Chato
waliojiandikisha kwenye daftari la kupiga kura walifika zaidi ya 200,000
na bila shaka wataenda kupiga kura, CCM tuna uwezo wa kuleta maendeleo
kwenye wilaya yenu, viongozi watakaochaguliwa wataenda kufanya kazi kwa sababu
ilani ipo, CCM wana ilani na mipango wengine hawana,” ameeleza Dkt. Biteko.
Aidha,
amesema tangu Rais Samia aingie madarakani CCM imekuwa na kauli mbiu ya kazi
iendelee huku ikiendeleza kwa juhudi kubwa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya
nchi.
Ametaja
miradi hiyo kuwa ni mradi wa kufua wa umeme wa
Bwawa la Julius Nyerere ambao sasa unafanya kazi, treni ya umeme ya
kisasa (SGR) inafanya kazi kutoka Dar es salaam hadi Dodoma, kuimarisha shirika
la ndege kwa kuongeza idadi ya ndege.
Fauka ya
hayo, Dkt. Biteko amesema CCM inaheshimu Uchaguzi huo wa Serikali Mtaa na ndio
maana viongozi wake wote wamesambaa katika maeneo mbalimbali kueleza umuhimu wa
uchaguzi huo.
“CCM tuna
sababu za kuomba kura kwa sababu tumepiga kazi na inaoonekana watu wa Chato
tupigie kura kuchagua wagombea wa CCM katika vitongoji vyote na vijiji hakuna
kumwachia mtu kwa kuwa wengine hawana ilani wala mipango,” amefafanua Dkt.
Biteko.
Mbunge wa
Chato, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa jitihada
zake za kuiletea maendeleo wilayani Chato.
Amebainisha
katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Chato imepata shilingi bilioni 197.28
kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo. “Tumepata shilingi milioni 100 kwa
ajili ya kujenga kituo cha mabasi, kwenye kituo cha afya Rais Samia ametupa
fedha kwa ajili ya kukikarabati.”
Amesisitiza
“Hapa Bwanga awali kulikuwa na shida ya umeme tunakushukuru sasa umeme umefika
katika vitongoji na vijiji 15. Nataka nikuhakikishie kwa fedha tulizopata za
miradi mikubwa kumi ikiwemo mradi wa uwanja wa ndege ambao unaendelea vizuri ndege
zinatua, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mipango na Fedha kimekamilika na mwezi ujao
kinafunguliwa, ujenzi wa maktaba ya kanda inayogharimu shilingi bilioni 7.2
ambayo imeshaezekwa.”
Amewahimiza
wananchi wa Bwanga kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa ili kuendeleza maendeleo Bwanga na Chato kwa ujumla.
0 Maoni