Kamishna wa
Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye
amesema Mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha inalinda, inahifadhi na inaimarisha
vivutio vya malikale inavyovisimamia.
Akizungumza
mara baada ya kutembelea Mapango ya Amboni mkoani Tanga yanayosimamiwa na
Mamlaka hiyo Dkt.Doriye amesema mapango ya Amboni ni moja ya vituo vya malikale
ambayo NCAA imedhamiria kuhifadhi, kuendeleza, kuboresha na kuyatangaza zaidi
ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea mapango hayo.
“Ziara yangu
katika mapango haya ni sehemu ya hatua za kuimarisha eneo hili ili kuongeza
chachu katika utalii wa malikale, juhudi kadhaa tumeshafanya katika eneo hili
ikiwepo uboreshaji wa njia za kupita ndani ya mapango, kuwekea taa ndani ya
mapango, tunaendelea na ujenzi wa geti, kuimarisha mifumo ya malipo na kuongeza
Ulinzi wa eneo lote la mapango, ” alisema
Dkt. Doriye.
Dkt. Doriye
ameongeza kuwa kwa sasa NCAA inaendelea kutanua wigo wa mazao mapya ya utalii
ili kuongeza vyanzo vya mapato na kuongeza mtawanyiko wa wageni hasa katika
vituo vya malikale.
“Tunamshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na
wizara yetu kwa kutuongoza vizuri katika kusimamia sera na mipango yetu ya
kuongeza vyanzo vya utalii na Mamlaka haitowaangusha viongozi wetu hao,”alisema
Dkt. Doriye.
Mapango ya
Amboni yamebeba historia kubwa ya harakati za kudai uhuru ambapo inaelezwa kuwa
baadhi ya wapinga ukoloni waliyatumia katika harakati za kudai uhuru wa nchi.
Mapango ya
Amboni ni moja ya vituo vya malikale vinavyosimamiwa na NCAA ambapo vituo
vingine ni eneo la Engaruka lililoko Monduli, Majabali ya Mumba yaliyopo
Karatu, Kimondo cha Mbozi Songwe pamoja na makumbusho ya bonde la Olduvai
lililopo Ngorongoro.
0 Maoni