Jeshi la
Polisi nchini limewakamata na kuwahoji watoto wawili kwa tuhuma za uharibifu za
kuvunja vioo viwili vya treni ya mwendo kasi inayotumia reli ya kisasa (SGR)
kwa kutumia mawe.
Taarifa
iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP David Misime imeeleza kuwa tukio
hilo lilitokea Novemba 22, 2024 majira ya mchana katika Kijiji cha Manase
Wilaya ya Chamwino katika Jiji la Dodoma wakati Treni ya Mwendo Kasi inapita
ikitokea Jijini Dar es Salaam kuelekea Jijini Dodoma.
Baada ya
tukio hilo kutokea, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kufanikiwa kuwakamata
Erasto Michael Richard (16) na Hassan Ezekiel Ndahani (12) wote wakazi wa
Kijiji cha Manase Wilaya ya Chamwino.
DCP David
Misime amesema chanzo cha kufanya uharibifu huo ni baada ya kuona treni ikipita
wakarusha mawe kwa pamoja ili kuona kama mawe waliyorusha yataweza kushindana
na mwendo wa treni.
Jeshi la
Polisi limetoa wito hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo treni ya kisasa
inapita kuendelea kupeana elimu juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya treni
hiyo kwani ipo kwa ajili ya manufaa ya wote.
0 Maoni