Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amempongeza Waziri wa
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa kwa kuunda
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari mapema mara baada ya kuteuliwa.
Balile
amesema hiyo ni hatua kubwa kwani imechukua miaka Nane tangu kutungwa kwa
Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 inayotamka uundwaji wa bodi hiyo.
Ametoa kauli
hiyo jana tarehe 21 Novemba, 2024 wakati akiwasilisha hoja za jukwaa hilo mbele
ya Waziri kwenye Kikao cha kwanza cha kufahamiana na Wajumbe wa Umoja wa Haki
ya Kupata Taarifa (CoRI) kilichofanyika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.
“Tunakushukuru
sana Mheshimiwa kwa sababu imechukua miaka Nane tangu Sheria imepita 2016 na Bodi ilikuwa haijawahi kuundwa na leo
tumesikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Bw. Patrick Kipangula, siyo mgeni sana
kwetu lakini leo tumemsikia kwa cheo kipya, tunashukuru sana na tunampongeza
sana,” amesema Balile akionesha kuridhishwa na Hatua hiyo ya Waziri Silaa
kuunda Bodi ya Ithibati.
Waziri Silaa
aliiteua Bodi ya Ithibati ya Waandishi
wa Habari Septemba 18 na kumteua Mwandishi wa Habari Nguli Tido Mhando kuwa
Mwenyekiti wa Kwanza na wajumbe wengine sita kutoka Taasisi za Habari kama
ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma za Habari.
Wajumbe wa
Bodi hiyo ni Bw. Thobias Makoba, Mgaya Kingoba, Dkt. Rose Reuben Mchomvu, Dkt
Egbert Mkoko na Laslaus Komanya.
Akizungumza
na Wadau wa Habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu
2025, tarehe 19 Novemba, Waziri Silaa alibainisha kuwa uzinduzi rasmi wa bodi
hiyo muhimu utafanyika mapema mwezi Disemba, 2024 na kwamba itafungua njia ya
safari ya kuanzisha Baraza Huru la Habari na pia Mfuko wa Mafunzo kwa
Wanahabari na tathimini ya hali ya uchumi kwa vyombo vya habari.
Katika hoja
yake Balile alimuomba Waziri kuwa na kikao kazi kitakachogusia Sera ya Habari,
Sheria na mfuko wa mafunzo ili kupata uelewa wa pamoja wa namna ya kuiboresha
tasnia ya Habari na Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Ombi kama
hilo pia liliwasilishwa na Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura aliyemuomba
Waziri katika vikao vijavyo kuwa na majadiliano ya namna Baraza Huru la Habari
lililoundwa na Sheria ya Huduma za Habari
litakavyoendesha majukumu yake ili kujitofautisha na Baraza la Habari
Tanzania (MCT) ili kuondoa mgongano.
0 Maoni