Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema Tanzania inakwenda kuandaa Tuzo za Utalii duniani (World Travel Awards, WTA) kwa Bara la Afrika kwa mwaka 2025.
Dkt. Abbasi
ametoa kauli hiyo leo Novemba 26, 2024 wakati akiongea na Vyombo vya Habari
mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kutoka nchini
Ureno ambapo Tanzania ilitwaa
Tuzo ya Dunia ya Sehemu Maridhawa
Zaidi kwa Utalii wa Safari 2024 (World’s Leading Safari Destination) usiku wa
kuamkia jana.
Dkt. Abbasi
amefafanua kuwa Tanzania imepata Tuzo hiyo kutokana na ushirikiano mkubwa wa
wadau mbalimbali wa Utalii nchini katika kutangaza vivutio vya utalii.
Aidha,
amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour
na Amazing Tanzania imesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.
Ameongeza kuwa
Tuzo hizo ni ishara ya kwamba
wageni wamekuwa na imani kubwa na
vivutio vya utalii na ukarimu ambao
wamekuwa wakipata wakati wanapokuja kutembelea vivutio hivyo na
kuwataka kuendelea kuwa wakarimu.
Ametoa
wito kwa watanzania wote
kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuhifadhi vivutio vya utalii na raslimali zilizopo ili
viweze kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru amesisitiza kuwa kwa
sasa Tanzania inakwenda kutangaza mazao mapya ya utalii ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii na hivyo kuwafanya wageni kuongeza siku za
kukaa na kutumia wakifika nchini.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi amesisitiza wadau wote
nchini kuzingatia sera na kanuni mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili sekta ya utalii
nchini iendelee kukua.
0 Maoni