Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka
wananchi wa Geita kujitokeza wa wingi kesho na kuchagua wagombea wa CCM.
Amewahimiza
wananchi hao kuendelea kumuunga mkono yeye na CCM ili kutoa fursa ya kuendeleza
jitihada za maendeleo “Nimekuja hapa kuwaambia msiniangushe wala kuiangusha CCM
kwa kuwa miradi na juhudi zote zinazoendelea zinalenga kuleta maendeleo kwenu.”
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Novemba 26, 2024 wakati akifunga Kampeni za Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Geita zilizofanyika katika Uwanja wa Mwenge,
Uyovu, wilayani Bukombe.
Ameongeza
kuwa kampeni za 2024 zimekuwa za kistaarabu huku akiwashukuru wanachama wa CCM
kwa kuendeleza kauli mbiu ya Rais Samia ya kujenga Taifa moja la kuheshimiana
na kustahimiliana.
Dkt. Biteko
amebainisha sababu za kuwaomba wananchi hao kuipigia kura CCM kuwa “Wana Uyovu nataka niwakumbushe kazi ambazo zimefanywa tangu mwaka 2015, Kata
hii ya Uyovu ilikuwa na shule za msingi tano, tumejenga saba sasa zipo 12,
zilikuwa shule za sekondari mbili, tunajenga zingine ili ziwe sita.”
Ameendelea
kusema Serikali inayoongozwa na CCM imeimarisha miradi ya maji, imejenga
barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.2 na pia katika Wilaya ya Bukombe
kitajengwa Chuo cha VETA.
Dkt. Biteko
amesema kuwa na vyama vya upinzani si vibaya, watu washindane kwa hoja na sio
kubaguana huku akiwataka wagombea wa CCM watakapochaguliwa wafanyekazi kwa
uaminifu na uwazi ili kuchochea maendeleo.
“Tunataka
uchaguzi huu uwe wa amani, wa kistaarabu na wa haki kusiwe na kubebwa,
uchaguzi huu usitufanye tugawanyike, ufanyike kwa amani na utufanye
tuwe wamoja na baada ya uchaguzi
tuijenge wilaya yetu, siasa ziwe
daraja la kutuunganisha na kushindanisha mawazo,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholous Kasandamila na Katibu wa Chama
Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Alexandrina Katambi kwa nyakati tofauti
wamewataka wanachama wa CCM kujitokeza
kwa wingi kwenda kupiga kura kesho na kuchagua wagombea wa CCM.
Naye,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja
amewashukuru wananchi wa Geita kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa
ufungaji kampeni.
Pamoja na
hayo Dkt. Biteko alishiriki Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
zilizofanyika katika Wilaya tano za Mkoa wa Geita ambazo ni Mbogwe, Chato,
Geita, Bukombe na Nyang’hwale.
Aidha, mkutano huo wa ufungaji kampeni umeambatana na burudani kutoka katika vikundi vya sanaa zaidi ya 40 pamoja na msanii mkubwa kutoka Kanda ya Ziwa, Magambo Machimu Lenga.
Kampeni za
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizinduliwa tarehe 20 Novemba, 2024 kwa
Viongozi mbalimbali wa CCM kufanya uzinduzi katika mikoa mbalimbali ambapo Dkt.
Biteko alizindua Kampeni hizo kwa Mkoa wa Mara.
0 Maoni