Katibu
Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogoro ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) kwa kuingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited
ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Mbeya kwa kuuza kwa bei ya
ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya
vijijini na pembezoni mwa miji.
Mpogoro
ametoa pongezi hizo leo Novemba 20, 2024 mkoani humo baada ya uwasilishwaji wa
taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya uzito wa kilo
sita iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na
Mbadala, Mha. Advera Mwijage.
Mpogoro
amesema kuwa mitungi ya gesi itakayosambazwa mkoani Mbeya itachochea kwa kiasi
kikubwa matumizi ya nishati safi na salama.
"Naipongeza
REA kwa kuja na mradi huu, naiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi
wengi nishati hii muhimu itakayokuwa mkombozi kwetu," amesema Mpogoro.
Mha. Mwijage
amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya
vijijini na pembezoni mwa mji.
"Lengo
la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za
nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti ambapo takribani hekta
400,000 hukatwa kila mwaka," ameongeza Mha. Mwijage.
Amezitaja
wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Mbeya, Chunya, Kyela,
Mbarali na Rungwe.

0 Maoni