Waziri wa
Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji
katika Sekta ya Madini unatarajiwa kuongeza fursa za uwekezaji katika Sekta ya
Madini hapa nchini sambamba na kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya
wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha kuwa rasilimali za
madini zinawanufaisha watanzania kiuchumi na kijamii.
Amesema hayo
leo Novemba 14, 2024 wakati akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari
Jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya Mkutano wa 6 wa Kimataifa wa
Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini Tanzania, unaotarajiwa kufanyika
kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa, Mkutano huo unaoongozwa na Kaulimbiu ya “Uongezaji Thamani Madini kwa
Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii” unatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki muhimu
Zaidi ya 1,500 kutoka Tanzania na nchi mbalimbali duniani na kwamba ni jukwaa
muhimu kwa wadau wa madini kubadilishana uzoefu, maarifa, na mikakati
mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Madini, maendeleo ya
taifa na uchumi kwa ujumla.
“Mkutano huu
ni jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana
maarifa, ujuzi na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua
kwa kasi. Pia, unatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu Sera na mikakati
mipya ya serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na
madini, na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi
katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini kupitia mawasilisho na
maonesho kwenye mabanda yanayoenda sambamba na mkutano,” amesema Mavunde.
Mhe. Mavunde amebainisha kuwa kaulimbiu ya mwaka
huu inalenga kuhamasisha uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida
zaidi za kiuchumi na kijamii kwa Tanzania na dunia kwa ujumla na kusisitiza
kuwa Serikali imejipanga kuhimiza uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini
ndani ya nchi ili kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania.
Waziri
Mavunde ameongeza kuwa, Mkutano huo utahudhuriwa na Viongozi wa Kimataifa
wakiwemo Mawaziri wa kisekta kutoka mataifa ya Afrika, wawakilishi wa Kampuni
kubwa za madini duniani, mabalozi 31 wanaowakilisha nchi zao hapa nchini,
pamoja na taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za madini kwa
kuwa Mkutano huo ni fursa ya kipekee kwa wawekezaji na wafanyabiashara
kuangalia nafasi za kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha, Mhe.
Mavunde amesisitiza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sekta ya madini na
kuhakikisha kuwa nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, Mkutano huo utaambatana na hafla ya
“Usiku wa Madini” mnamo tarehe 20 Novemba, 2024, halfla inayohusisha utoaji wa
tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika ya Sekta ya Madini sambamba na maonesho
ya bidhaa za madini, ikiwa ni pamoja na vito vya thamani huku ikionyesha nafasi
ya madini katika maisha ya kila siku ya Watanzania.
Mkutano huo,
unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 19 Novemba 2024, huku ukitarajiwa
kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi mnamo tarehe 21 Novemba 2024.
0 Maoni