WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameagiza kuwa mitaala inayoandaliwa ihakikishe inazingatia
mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya kiteknolojia.
Amesema hayo
leo, Novemba 22, 2024, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi linalifanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma.
Amesema kuwa
kuna umuhimu wa kutumia teknolojia katika kuboresha elimu ya biashara kwa
kutumia jukwaa la mtandao kutoa mafunzo ya biashara, matumizi ya programu za
kisasa za biashara, na kupanua matumizi ya teknolojia katika biashara na
ujasiriamali. “Hivyo, nitoe rai kwa taasisi za elimu na mafunzo ya biashara
kujikita katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo.”
Pia,
ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau
waendelee kuimarisha na kuboresha mifumo ya elimu ya biashara katika ngazi zote
za shule na vyuo na kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Katika Hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Taasisi za elimu na mafunzo ya biashara
zihakikishe zinakuza ushirikiano na sekta binafsi ili kusaidia katika kubaini
mahitaji halisi ya soko na kutoa mafunzo na elimu inayoendana na mabadiliko ya
sekta ya biashara.
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa biashara si tu
zinanufaisha wamiliki, bali pia zinachangia katika maendeleo ya kijamii na
kiuchumi. “Biashara zinapaswa kuchangia katika kulinda mazingira na ustawi wa
jamii.”
Kw upande
wake Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa kongamano
hilo maalum la kitafiti litasaidia kuibua mijadala itakayowezesha kubaini
changamoto na fursa zitazoisaidia nchi kupata mafanikio katika sekta ya
biashara na uchumi.
“Kwa takwimu
za mwaka 2001 vijana waliomaliza vyuo vikuu, walikuwa 51800, na kadiri miaka
inavyoenda ndivyo wanavyoongezeka, Serikali pekee haiwezi kuajiri, tunategemea
wengine waende sekta binafsi, tunazo fursa za masoko kwenye nchi za SADC,
Afrika Mashariki, na la huru za afrika; ili kuweza kuyafikia masoko hayo lazima
tufanye tafiti.”
Naye, Mkuu
wa chuo cha Elimu ya Biashara Prof. Edda Tandi Lwoga, amesema kuwa wamefanikiwa
kuongeza bajeti ya utafiti kutoka milioni 46 mwaka 2018 hadi milioni 300 mwaka
wa fedha 2023/2024.
“Kipindi cha
miaka mitano, Chuo kimefanikiwa kuchapisha jumla ya machapisho 288 katika
majarida ya kitaifa na kimataifa, kutokana na juhudi za wahadhiri na watafiti
wetu katika kuendeleza elimu na kuzalisha maarifa mapya.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua kitabu cha tafiti za biashara 114 zilizoandaliwa na watafiti mbalimbali wa masuala ya biashara, kwenye ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma Novemba 22, 2024. Kutoka kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Saidi Jafo, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dkt. Kennedy Hosea, Mkuu wa chuo cha Elimu ya Biashara Prof. Edda Tandi Lwoga. Waziri Mkuu alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano hilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


0 Maoni