Katibu Mkuu
wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Ismail Samamba amewataka Maafisa Madini
Wakazi wa Mikoa kuweka nguvu kwenye usimamizi wa usalama na mazingira kwenye
migodi ya madini hasa katika msimu huu wa mvua ili kuepuka ajali zinazoweza
kutokea na kusababisha vifo.
Mhandisi
Samamba ametoa agizo hilo leo Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye
kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini ikijumuisha Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Janet Lekashingo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani
Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
“Ninawataka
kufanya ukaguzi mkubwa kwenye migodi yote ya madini nchini hasa katika kipindi
hiki cha mvua na kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo
hatarishi ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua
nyingine,amewapongeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa mwenendo bora wa
ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na
kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
“Katika
kipindi cha kwanza cha mwaka wa fedha 2024/2025 mwenendo wa makusanyo ya
maduhuli ambapo mpaka sasa wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 395
zimeshakusanywa, nawapongeza kwa kazi nzuri sana na kuwataka kuongeza ubunifu
kwenye ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kushuka kwa
bei ya dhahabu kwenye soko la dunia na kipindi cha mvua ambacho kinatarajiwa
kuanza hivi karibuni,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.
Katika hatua
nyingine amewataka maafisa hao kutoa elimu kwa wadau wa madini kuhusu fursa za
uwekezaji katika Sekta ya Madini katika mikoa yao kupitia warsha, maonesho na
makongamano mbalimbali.
Aidha, amewataka kuendelea kusimamia kwa karibu
watumishi waliopo chini yao na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea
kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kutosha na
uboreshaji wa maslahi ya watumishi.
0 Maoni