Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt.
Doto Biteko amesema kuwa kwa miaka yote wananchi wa Wilaya ya Bukombe wamekuwa
na imani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kiu ya maendeleo.
Amesema
wananchi hao wana haki ya kuchagua kati ya maneno au maendeleo na wamekuwa
wakitamani maendeleo kwa kuwa na shule, barabara na zahanati.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Novemba 21, 2024 wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Bukombe zilizofanyika katika Kata ya Igulwa,
Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita.
“Tunapozindua
kampeni zetu tuna wajibu wa kuchagua maneno au maendeleo, tutashindanisha vyama
kwa sera na kuonesha tuliyofanya kwa kipindi kilichopita. Tumekuja leo
kuwaambia sisi tuko upande wa maendeleo na wengine wako upande wa maneno kama
mwakilishi wenu nimekuja kuwaambia tuchague maendeleo, tuchague CCM,” amesema
Dkt. Biteko.
Amesisitiza
“Tuliwahi kupata viongozi wa chama kingine na sasa tuna wajibu wa kupima kati
yao na CCM mabadiliko yako chama gani,”
Akielezea
hali ya uandikishaji wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa, amesema
kuwa mwaka 2024 Bukombe imefanikiwa kuandikisha idadi kubwa ya wapiga kura
ambayo ni 228,659 ikiwa ni rekodi ya juu katika mkoa na ukanda huo hali
inayodhihirisha ushindi kwa CCM na hasa kutokana na utekelezaji wa ilani yake.
Halikadhalika,
Dkt. Biteko amesema asilimia 70 ya vitongoji vina wagombea wa CCM huku vyama
vingine vikishindwa kuweka wagombea.
“ Novemba
27, 2024 wote tukapige kura tunatakiwa kumshukuru Rais Samia kwa upendo na kwa
kufanya jitihada nyingi za kutujengea
barabara, shule za msingi na sekondari, vyuo vya VETA, shule ya amali na
mengineyo kwa haya yote twende tukawapigie kura wagombea wa CCM,” amesema Dkt.
Biteko.
Pamoja na
hayo amewaasa wananchi wa Bukombe kuhubiri umoja, amani na upendo hata baada ya
uchaguzi kuisha sambamba na wagombea hao kuhudumia wananchi wa Bukombe.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amesema kuwa kazi
ya CCM katika uchaguzi ni kushinda kwa ngazi zote za kata, vijiji, vitongozi.
Katibu wa
Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Alexandrina Katabi amewataka wanachama wa
CCM Wilaya ya Bukombe kuendelea kuimarisha umoja na ushirikiano wao hasa wakati
huu wa kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Diwani wa
Kata ya Bugelenga, Leonard Lubigisa akizungumza kwa niaba ya madiwani amewataka
wanachama wa CCM kupiga kura ifakapo Novemba 27, 2024.
Aidha,
ameipongeza Serikali kwa kuendelea kupelekea maendeleo katika Jimbo hilo na
kuhamasisha wananchi kuichagua CCM kwa jitihada zake za ujenzi wa barabara
pamoja na miradi mingine.

0 Maoni