Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameipongeza Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kwa kuandikisha idadi kubwa ya wananchi katika daftari la wapiga
kura ikiwa ni maandalizi ya Uchanguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa
kufanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Biteko
ametoa pongezi hizo leo Novemba 10, 2024 wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi wa Jimbo la Dodoma Mjini uliyolenga kutoa Taarifa ya
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa Mwaka 2020 hadi 2024.
“Kipekee
kabisa niwapongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya vizuri zaidi
kuliko Halmashauri yoyote nchini kwa uandikishaji uliovuka lengo mpaka kufikia
asilimia 128 ya lengo la uandikishaji. Hii ni kuthibitisha kwamba Mkoa wa
Dodoma mmejipanga vizuri sana kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
Uchaguzi Mkuu ujao,” amesema Dkt. Biteko.
Pia, Dkt.
Biteko ametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri
wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambayo imeleta manufaa makubwa katika ustawi wa jiji la Dodoma.
“Ninampongeza
sana Mbunge wenu Mhe. Anthony Peter Mavunde kwa tukio la leo la uwasilishaji wa
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024
pamoja na kukabidhi vitendea kazi kwa viongozi kwa ajili ya maandalizi ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nimefurahishwa kwa namna ambavyo zimefanyika
kazi kubwa za kugusa maisha ya watu na hasa watu wenye kipato cha chini na kuwa
karibu na wananchi,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza
“Nataka niwaambie watu wa Dodoma Mhe. Mavunde ana sifa nyingi nataka nitaje
chache, Mbunge wenu anajua ubunge alionao si wake ni wa CCM na wanachama wake
hivyo wakati wote amekuwa mtu anayeshughulika na shida za watu, mtu anayefanya
kazi na anastahili kuambiwa akiwa hai yeye anafanana na watu walipewa talanta
na yeye anafanana na aliyepewa talanta
tano.”
Aidha, Dkt.
Biteko ametoa wito kwa wananchi wa Dodoma Mjini kuendelea kumpa ushirikiano
mbunge wao ili aendelee kutimiza majukumu yake ipasavyo sambamba na kuwataka
wananchi hao na kutunza amani wakati wa uchaguzi.
“Tunapokwenda
kwenye uchaguzi watu wa Dodoma mmejipanga, Dodoma Jiji imeandikisha watu
628,000, umefanyika utekelezaji mzuri wa Ilani haya yote yamefanyika kwa zaidi
ya asilimia 90, na CCM imefanya uhamasishaji mkubwa wakati wa kujiandikisha
kwenye daftrari la kupiga kura hivyo hizi ni sababu za kutupa ushindi, wakati
wa uchaguzi tuikatae roho ya mgawanyiko na tushikamane kwa ajili ya kujenga
chama na na nchi yetu,” ameeleza Dkt. Biteko.
Ameendelea
kuwahimiza wana CCM kuwa chama chao ni chama kiongozi na kuwa waendelee
kuhamasisha Watanzania kuendeleza misingi ya upendo, mshikamano na umoja
sambamba na kuwa na upendo kwa vyama vingine vya siasa.
Fauka ya
hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuipa kipaumbele Dodoma kama
Makao Makuu ya nchi kwa kuendeleza na kuanzisha miradi mingi
itakayofanana na sifa ya makao makuu ya nchi na kuwa wananchi wa Dodoma
waendelee kuwa na mshikamano kwa kuwa Serikali inatambua mahitaji yao na
inaendelea kuyafanyia kazi.
“Tunashuhudia kukamilika kwa ujenzi wa Mji wa
Serikali Mtumba ambapo Watanzania wote watapata huduma za Serikali katika eneo
moja na hivyo kuwaondolea usumbufu kama ilivyokuwa awali kutokana na mtawanyiko
wa Ofisi za Serikali. Tunashukuru ujenzi wa Kiwanja kikubwa cha Ndege cha
Msalato ambacho kwa sasa ujenzi wake umefika zaidi ya asilimia 75. Kukamilika
kwa kiwanja hiki kutasaidia kurahisisha usafiri kwa wananchi wetu na kuchochea
maendeleo ya Dodoma na maeneo ya karibu,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Akitoa
Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi
cha Mwaka 2020 hadi 2024, Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,
Mhe. Anthony Mavunde amewashukuru wananchi wa Jimbo hilo kwa kumchagua na
kuendelea kumpa ushirikiano katika kazi zake.
Amesema kuwa
Jimbo lake katika kipindi cha miaka minne limepokea zaidi ya shilingi trilioni
1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ametaja
baadhi ya miradi inayotekelezwa katika Jimbo lake ambayo ni ujenzi wa barabara
ya pete yenye urefu wa km 112.3 inayojengwa Dodoma ili kuondoa msongamano wa
magari na ujenzi wa uwanja wa kudumu kwa ajili ya Maonesho ya Wakulima ya
Nanenane.
Ameongeza
kwa kusema “Mhe. Rais Samia ametoa maelekezo unajengwa uwanja mkubwa wa mpira
wa miguu hapa Nzuguni, Dodoma. Kwenye vituo vya afya na zahanati tumepokea
fedha nyingi na kazi nyingi zinaendelea sambamba na ujenzi wa hospitali mpya ya
wilaya inayojengwa katika Kata ya Nala.”
Mhe. Mavunde
ameendelea kutaja miradi mingine ambayo ni nishati ya umeme na kusema kuwa
awali katika Kata ya Chihanga na Mbawala hakukuwa na nguzo za umeme na sasa
kuna nguzo za umeme na kuwa yamebakia maeneo machache ili umeme usambazwe katika jimbo la Dodoma Mjini.
Akizungumzia
utekelezaji wa ahadi zake katika Jimbo hilo, amesema kupitia fedha za Mfuko wa
Jimbo amegawa zaidi ya matofali 80,000 na mifuko ya saruji elfu 15 katika kata
zote ili kuchochea ujenzi wa zahanati.
“Nimegawa
mashine za kutotolesha vifaranga kwa akina mama ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha
kiuchumi, katika elimu tumegawa vishikwambi kwa walimu vyenye gharama ya
shilingi bilioni 1.7, nimegawa kompyuta 102 katika shule za msingi na
sekondari,” amesema Mhe. Mavunde.
Amesisitiza
“Nimejenga Shule ya Msingi Chiwondo ili kusaidia wanafunzi waliokuwa wakitembea
umbali mrefu kutafuta shule, watoto waliokuwa wanasoma Shule ya Sekondari Ipala
niliwahidi nitajenga shule na sasa shule imejengwa na imekamilika.”
Pia,Mhe.
Mavunde amesema kuwa Jimbo lake lilikuwa na changamoto kubwa ya ardhi lakini
kupitia kliniki za ardhi zilizofanyika zimesaidia kutatua changamoto hiyo kwa
kiasi kikubwa.
Naibu Waziri
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainab
Katimba amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uwekezaji
mkubwa katika Jimbo la Dodoma Mjini hususan katika miundombinu ya barabara.
“Katika
miundombinu ya barabara mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka minne
tumeona ongezeko la bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 5.3 hadi 42.6 kwa
mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu, hii ni dhamira ya dhati ya Rais kuona
Dodoma inapata miradi ya kimakakati,” amesema Mhe. Katimba.
Amebainisha
“ Sasa TARURA inaweza kuhudumia mtandao wa barabara za lami kutoka urefu wa km
154 hadi km 249 na barabara za changarawe
kutoka km 196.4 hadi km 368.2 hapa Dodoma Mjini, imejenga makaravati 9 pamoja na kupamba jiji hili kwa
taa za barabarani 243.”
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Charles Mamba
amesema kuwa mkutano huo ndio ulimpendekeza Mhe. Anthony Mavunde kufanya kazi
za kibunge na kupitia mkutano huo pia ataeleza yale ambayo ametekeleza katika
Jimbo hilo.
Ameongeza
kuwa Dodoma Mjini wako tayari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
wamedhamiria kushinda nafasi za uenyekiti kwa asilimia 100.
Awali, Dkt. Biteko amekabidhi baiskeli 223 kwa makatibu wa matawi wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na spika 45 kwa makatibu kata wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Dodoma Mjini ikiwa ni jitihada za Mbunge wa Jimbo hilo kusaidia viongozi hao kuwafikia wananchi kwa urahisi pamoja na kuwezesha ufanyikaji wa mikutano ya hadhara kwa wananchi.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni