WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa vitakavyoshiriki
katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuwa vinara katika kulinda amani na
kukemea viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.
“Hamasisheni
wanachama wenu kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia kudumisha amani
iliyopo. Wananchi wote waliojiandikisha katika orodha ya wapigakura wa Uchaguzi
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wajitokeze kwa wingi kupiga kura katika vituo
vyao siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024. Siku hiyo itakuwa ya mapumziko
maalum kwa ajili ya uchaguzi huo.”
Ametoa wito
huo leo (Jumapili, Novemba 10, 2024) wakati alipomwakilisha Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu na Kongamano la Umuhimu wa Amani
kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam. “Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia amewasihi Watanzania na viongozi wa dini kuendelea kuitangaza amani
ndani na nje.”
Katika
Kongamano hilo, ambalo linaratibiwa na Jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Shia
Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi hao
kuhamasisha wanachama wao kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia suala
la kudumisha amani kwa muhimu mkubwa.
Mheshimiwa
Majaliwa amesisitiza kwamba kila Mtanzania mwenye sifa ajitokeze kupiga kura
ili kuwachagua vongozi ambao ni
mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe wa
serikali za vijiji na kamati za mitaa. “Ikumbukwe kuwa kupiga kura ni wajibu na
haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania.”
Aidha,
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini kazi
kubwa inayofanywa na madhehebu ya dini pamoja na taasisi zote, ambapo licha ya
kutoa mafundisho ya kiroho, taasisi za dini zimekuwa zikiunga mkono jitihada
mbalimbali za Serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.
Kwa Upande
wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania Alhad Mussa Salum
ameipongeza Jumuiya ya Waislam wa Shia Tanzania kwa harakati zake za
kuhakikisha amani na utulivu wa Tanzania unaendelea kukua. Mimi ni shuhuda
mzuri wa harakati za Shia wanazofanya ili kuhakikisha amani na usalama wa
Tanzania unaendelea kuimarika.
0 Maoni