Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amehimiza upendo, amani na ushirikiano miongoni
mwa wananchi wa Sengerema ili waweze kujiletea maendeleo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Novemba 1,
2024 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la soko la
zamani, wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
“Tumekutana hapa kwa kuwa nchi ina
amani, watu wa Sengerema tupendane, tushirikiane, tuthaminiane na tujaliane ili
tuweze kuwa na fursa ya kujishughulisha na shughuli zitakazotuletea maendeleo,”
amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Mhe. Rais amefanya mambo
mengi na alipopita hapa alieza, tunapotaja miradi aliyotekeleza tunamtaja sana
yeye Mhe. Rais kwa sababu dhamana ya maendeleo ya Watanzania na wananchi wa
hapa Sengerema ipo mikononi mwake.”
Dkt. Biteko ameendelea kwa kusema
Sengerema haikuwahi kuwa na hospitali ya wilaya isipokuwa katika kipindi cha
Rais Samia imepata hospitali hiyo. Amefafanua zaidi kwa kusema alipoitembelea
hospitali hiyo amebaini upungufu wa majengo ambayo ni jengo la upasuaji na kuwa
fedha kwa ajili ya ujenzi wake zimeshatolewa tayari, fedha za jengo la wagonjwa
mahututi nazo zimefika wilayani hapo na kusema kuwa ujenzi wa uzio wa hospitali
utafanyika kwa kutumia mapato ya ndani ya wilaya.
Akizungumzia umeme katika Wilaya ya
Sengerema, amesema kuwa vijiji vyote 71 vimepata umeme na kuwa katika vitongoji
425 ni vitongoji vicheche havina umeme na vinafanyiwa kazi ili wilaya hiyo
ipate umeme wa uhakika, Dkt. Biteko amesema Serikali inajenga njia nyingine ya
umeme kutoka Nyakanazi hadi Igaka na kutoka Igaka hadi Sengerema na kuwa
jitihada hizo za Serikali zinatafsiri maendeleo ambayo yanahitajika na watu wa
Sengerema na sio maneno pekee.
Aidha, amewapongeza wananchi wa
Sengerema kwa kuwa na jitihada katika kuzalisha chakula cha kutosha ambapo
wamezalisha zaidi ya tani 500,000 huku mahitaji yakiwa tani 333,000 pekee.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema
kuwa wananchi wa Sengerema wamempata mbunge mchapakazi Mhe. Hamisi Tabasamu na
kumtaka aendeleze juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi wake sambamba na
kuwahimiza wananchi kuendelea kumpa ushirikiano zaidi mbunge huyo.
Pia, Dkt. Biteko amewaasa wananchi wa
Sengerema kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na kufuata taratibu
na sheria na kuwa uchaguzi huo usiwe sababu ya kuwagawa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.
Said Mtanda amesema kuwa Mkoa wake umejiandaa vizuri kwa ajili ya kushiriki
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwa umeshika nafasi ya tatu katika zoezi la
kuandikisha wapiga kura kwa idadi kubwa katika Daftari la Wapiga Kura.
Kwa upande wake, Diwani Kata ya
Ibisawageni, Mhe. Jumanne Masunga ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa
ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo
kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya
sekondari katika kata yake.
“Hata katika miradi ya maji katika
wilaya yetu inaendelea vizuri sasa tumetandaza mabomba kama kilomita 75 ili
maji yaweze kuwafikia wananchi wetu. Mwaka jana tumejenga tanki la maji kwa
kiasi cha shilingi milioni 554 na tunajenga barabara ya lami, tunaomba
utufikishie shukrani zetu kwa Rais Samia na tunamuomba atuongezee bajeti ya
ujenzi wa barabara za lami,” amesisitiza Bw. Masunga.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni