Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wahitimu katika ngazi mbalimbali kutumia taaluma yao kufanya maamuzi sahihi yatakayowawezesha kupata majibu ya maswali na dukuduku walizonazo kuelekea maisha mapya.
Dkt. Biteko
ametoa rai hiyo Novemba 16, 2024 katika Mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu Kishiriki,
Stella Maris cha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mtwara.
Pamoja na
kuwapongeza wahitimu kwa kuhitimu amewataka kutumia taaluma waliyoipata kuwa
nyenzo katika utatuzi wa changamoto watakazokabiliana nazo maishani baada ya
kuondokana na maisha ya chuo.
“Wengine
wanaendelea kujiuliza, nini kitafuata baada ya kuhitimu? Uelekeo utakuwa ni
upi? na wengine wanasema hali sio nzuri huko tuendako. Kila wakati endelea kuwa
tofauti, kila mtu ana njia yake ya kuishi, tumia taaluma mliyoipata kwa maamuzi
sahihi. Amini vyeti pekee havitoi maarifa bali endeleeni kujifunza kwa
waliowatangulia,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko
amewapa shime wahitimu na kuwataka wasisikilize sauti za baadhi ya watu wenye
nia ya kuwavunja moyo kwa vitisho na kauli za kukatisha tamaa kuhusu maisha
baada ya kuhitimu elimu ya Chuo.
“Acheni
kusikiliza kauli za wavunja moyo bali fuata sheria, tenda haki na kumjenga
mwenzako kimaisha na kisaikolojia,’’amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua
nyingine, amewataka wahitimu kujipanga na kukabiliana na matokeo ya ushindani
pamoja na matishio mbalimbali ya kidunia ikiwemo mabadiliko ya teknolojia na
changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ongezeko la joto
duniani, ongezeko la idadi ya vimbunga, ukame, njaa na matetemeko ya ardhi.
Awali, mgeni
rasmi amesema serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa sekta binafsi katika
kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo sekta ya elimu.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Mhashamu Askofu Titus Mdoe ameishukuru
Serikali kwa kutoa kibali, miongozo na ushauri katika uendelezaji wa shughuli
za elimu jambo linalowezesha utekelezaji wa malengo waliojiwekea.
“Tunaishukuru
Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suhuhu Hassan pamoja na viongozi
wengine kwa ushirikiano tunaoupata kutoka ngazi ya wilaya hadi Taifa,” amesema
Askofu Mdoe.
Mwenyekiti
huyo wa Bodi ya Chuo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Agustine,
Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa ameiomba Serikali kuwashika mkono wanafunzi wa
Chuko Kikuu Kishiriki cha Stella Maris ili waweze kutatua changamoto za maisha
wanapokuwa chuoni.
Naye Mkuu wa
Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara, Padri, Profesa Thadeus Mkamwa
amesema elimu inayotolewa katika chuo hicho kuwajengea wanafunzi uwezo na
umahiri katika utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo.
Pia amesema
wanachuo wanafundishwa misingi ya upendo, uvumilivu pamoja na kuwajengea vijana
mifumo ya ubunifu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Jumla ya
wanachuo 581 wamehitimu wakiwemo wa ngazi ya astashahada, stashahada pamoja na
shahada ikiwa ni sawa na asilimia 83 ya waliostahili kuhitimu huku wanafunzi
117 wakishindwa kuhitimu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa
ada.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni