Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana
(Mb) amezindua nembo ya asali ya Tanzania itakayotumika kuitambulisha bidhaa
hiyo katika soko la dunia huku akitoa rai kwa Wafanyabiashara kuchangamkia
fursa ya kuuza asali nchini China.
Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 4, 2024 katika Chuo cha
Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora (BTI), Mkoani Tabora.
”Kupitia mradi wa BEVAC imeandaa nembo ya asali ya Tanzania
(Tanzania Trade Mark). Uwepo wa nembo hii utawahakikishia walaji kuwa bidhaa
watakayoitumia iko salama na inakidhi viwango vya ubora,” Mhe. Chana amesisitiza.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Chana ametoa rai kwa
wafanyabiashara wote wa asali ndani na nje ya nchi kuanza kuitumia nembo hiyo
ya ubora huku akiielekeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – Tan Trade
yenye jukumu la kusimamia matumizi ya nembo kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili
waweze kufahamu faida za matumizi ya nembo hii.
Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi
kwa wafugaji nyuki kwa kutenga maeneo maalum ya kufugia nyuki (Hifadhi za
Nyuki); na kujenga viwanda nane (8) vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki
katika Mikoa ya Tabora, Iringa, Katavi, Singida, Geita na Kigoma.
Vilevile amesema Serikali imeendelea kutafuta masoko mapya
ya asali nje ya nchi, ambapo Julai 15, 2024 Tanzania imesaini Itifaki na nchi
ya Jamhuri ya Watu wa China inayoruhusu asali ya Tanzania kuuzwa katika masoko
ya China.
”Nitumie nafasi hii kuwataka wafanyabiashara wote wenye nia
ya kuuza asali China kuwasiliana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ili
kupewa utaratibu wa kuuza asali nchini China,” amesema Mhe. Chana.
Sambamba na hilo, Waziri Chana ameweka jiwe la msingi katika
Jengo la bweni la wanafunzi wasichana la Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki
Tabora ambalo litagharimu Shilingi bilioni 2.65 sawa na Euro 954,314.4 na
ujenzi wake utatumia muda ya miezi 12.
Amesema hatua hiyo inachochea ushiriki wa wasichana katika
maendeleo ya sekta ya nyuki na kutumia fursa hiyo kutoa rai kwa wasichana
kuchangamkia fursa hiyo na kujiunga na masomo katika Chuo cha Mafunzo ya
Ufugaji Nyuki Tabora ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa au
kujiajiri.
Mhe. Chana ameushukuru Umoja wa Ulaya Tanzania kwa kuendelea
kuunga mkono juhudi za serikali za kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki nchini na
Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL), Kituo cha Biashara cha Kimataifa ITC
kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo.
Tanzania inazalisha wastani wa tani 33,276 za asali na tani 1,913 za nta kwa mwaka. Kiwango hiki bado ni kidogo ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji wa asali ambao unakadiliwa kuwa tani 138,000 kwa mwaka. Hata hivyo, kiwango cha asali kinachozalishwa kwa sasa kinaiweka Tanzania katika nafasi ya 14 duniani, nafasi ya Pili Afrika na nafasi ya Kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC.
Na. Happiness Shayo-Tabora
0 Maoni