Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko
amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa viongozi wa dini wanaoeleza waumini
wao kuhusu maendeleo kwa kuhimiza umoja, amani na mshikamano miongoni mwa
Watanzania.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2024 katika Misa Takatifu
ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre wa Dkt.
Faustine Kamugisha iliyofanyika Kijiji cha Kyamulaile, Wilaya Bukoba Mkoani
Kagera.
“Serikali yetu inathamini sana mchango wa viongozi wa dini
wanaoelekeza watu kwenye maendeleo ili tujenge nchi ya watu wanaopendana na kuthaminiana,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Kuwa na dini tofauti kwetu si tatizo, umoja
wetu tuutunze tuendelee kukumbushana kuwa hatuna taifa lingine na mwaka huu
tutakua na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tunadi sera zetu kwa ustaarabu.”
Dkt. Biteko ametoa wito kwa waumini wa Parokia ya Minziro
kuendelea kushirikiana na kumsaidia Padre Kamugisha ili afanye kazi yake ya
utume vizuri “ Wakatoliki wote na sisi
sauti zetu zikawe za kumfariji Padre huyu, ziwe sauti chanya kwenye
utume wake.”
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa salamu za Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa anamtakia
Padre huyo kila la heri na anampongeza kwa kazi kubwa anayofanya katika kanisa
na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa
amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini ikiwemo Kanisa Katoliki huku
akishukuru mchango wa kanisa hilo katika huduma za jamii.
“Tunatambua na kuthamini mchango wenu katika elimu kwa kutoa
elimu bora na shule za kanisa hili zimekuwa zikifanya vizuri na kwa upande wa
hospitali mfano Hospitali ya Kagondo imekuwa ikitoa huduma bora kwa wananchi,
imetupa chachu na sisi kuboresha hospitali yetu,” amesema Mhe. Mwassa.
Askofu Mkuu wa Jimbo la Bukoba, Jovitus Mwijage amempongeza
Padre Faustine Kamugisha kwa kutimiza miaka 25 ya upadre na kusema kuwa Padre
huyo amekuwa na juhudi katika kufanya utume wake na kujiendeleza katika masuala
mbalimbali.
“Tunakushukuru na kumshukuru Mungu kwa zawadi aliyokupatia,
utume huu usiishie hapa uendelee na sisi tutakukumbuka katika sala ili hudumu
katika utume huu,” amesema Askofu Mwijage.
Pia, Askofu Mwijage amesema kuwa Tanzania ni nchi isiyo na
dini ila watu wake wana dini hivyo amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na viongozi
mbalimbali wa Serikali kwa kuhudhuria katika misa hiyo jambo linaloashiria
umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akitoa shukrani zake, Padre, Dkt. Faustine Kamugisha
amemshukuru Mungu kwa kumsaidia kufikia hatua hiyo ya kutimiza miaka 25 ya
upadre.
Aidha, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na
Serikali kwa ujumla kwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Kanisa na Serikali hata
alipoomba umeme na maji katika vituo vya hija Serikali iliweza kusaidia
kufikisha huduma hizo.
Sambamba na kuwashukuru Maaskofu mbalimbali waliomsaidia
katika kufikia hatua ya miaka 25 ya upadre, amemshukuru pia Dkt. Biteko kwa
kuhudhuria misa hiyo.
Padre wa Jimbo la Tanga, Jonathan Mutalemwa wakati akihubiri
katika misa hiyo amesema kuwa kufikia siku hiyo ni ahadi ya Mungu na kuwa tukio
hilo ni muhimu kwa kuwa ni kitu ambacho baba yake mzazi Padre Kamugisha
alikitamani maishani mwake.
“Tunapofanya jubilei hii leo tujue famili ni kanisa dogo,
huyu tunamsheherekea leo ni Timotheo kwa kuwa imani aliyonayo na ujasiri
ulianzia kwa mzazi wake ambaye alifanya shughuli nyingi za kusaidia Kanisa
Katoliki Jimbo la Bukoba,” amesema Padre Mutalemwa.
Ameongeza kuwa sherehe hiyo ni ishara ya kuwa Padre
Kamugisha ameacha alama katika utume wake wa kazi ya ukuhani katika kipindi chote cha miaka 25.
Sambamba na misa hiyo ya Jubilei ya Miaka 25 ya Padre Kamugisha, Dkt. Biteko amezindua kitabu kinachoitwa “ Hatupangi Kushindwa, Tunashindwa Kupanga” kilichoandikwa na Padre huyo.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni